Gharama kubwa za matibabu katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi mkoani Kilimanjaro zinadaiwa kuwaweka njia panda baadhi ya wagonjwa wanaofika kupata huduma za tiba hospitalini hapo.
Baadhi ya wagonjwa hulazimika kutoroka hospitalini hapo na wengine kutelekezwa na ndugu zao kutokana na gharama kubwa wanazopaswa kulipia.
Mtoto Frank aliyelazwa katika wodi ya wagonjwa wa idara ya Upasuaji ambaye alifanyiwa upasuaji wa tumbo hivi Karibu anatajwa kuwa ni miongoni mwa wagonjwa waliotelekezwa hospitali hapa kwa zaidi ya wiki sasa kutokana na wazazi wake kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Dokta Kondo Chilonga ni daktari bingwa wa upasuaji na mkuu wa idara ya upasuaji katika hospitali hii kongwe ya KCMC, yeye alisema kutokana maisha kuwa magumu baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa wagonjwa wameshindwa kumudu gharama za matibabu na hivyo kuwalazimu wagonjwa waendelee kubaki hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Amos Makalla aliyezuru katika hospitali hiyo kwa lengo la kujionea changamoto zilizopo ikiwemo gharama kubwa za matibabu kwa pamoja ameahidi kuzifikisha changamoto hizo serikali ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Pamoja na mambo mengine ,hospitali ya rufaa ya kcmc inakabiliwa na ongezeko la wagonjwa hali inayolazimu baadhi ya wagonjwa kulala kwenye korido.