Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dokta Rajabu Rutengwe amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Wilaya ya Ulanga na kukuta malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya upungufu wa dawa na vifaa tiba hatua inavyokwamisha upatikanaji wa huduma bora kwenye hospitali hiyo.
Wananchi hao wamesema kwa muda mrefu hospitalihiyo imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa kitendo kinachowaathiri kwani hulazimika kuingia kwenye maduka ya mitaani kwa ajili ya kutafuta dawa ambazo zinakosekana hospitalini hapo.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro aliwasili katika katika mhospitali ya Wilaya ya Ulanga, ili kujua changamoto zinazoikabili hospitali hiyo, na kuangalia kama watumishi wake, wapo kwenye vituo vyao vya kazi.
Dokta Rutengwe aliwakuta watumishi wote wapo katika maeneo yao ya kazi, kikubwa anachokumbana nacho ni malalamiko kutoka kwa wananchi, juu ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba.
Dokta Rutengwe ameitaka serikali ya Wilaya kukaa na baraza la madiwani wa halmashauri hiyo na kuandaa bajeti itakayojitosheleza katika upatikanaji wa dawa kwa hospital hiyo, huku akiiomba MSD, kuwasilisha mapema dawa zinazoombwa na uongozi wa hospital hiyo.
Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, imekuwa tegemeo kwa wakazi waishio wilayani humo, kwani ndiyo hospitali ambayo imekuwa ikitoa vipimo na matibabu kwa wagonjwa wanaotoka katika tarafa zote za wilaya hiyo.