Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoani
Mara wameanza kuyakimbia makazi yao na wengine kulazimika kulala nje na
familia zao nyakati za usiku, baada ya nyumba zao kadhaa kubomolewa na
kundi la vijana wa Kikurya maarufu kama Saiga linalodaiwa kutekeleza
vitendo vya uhalifu, vikiwemo vya uporaji wa mali na fedha kwa mwavuli
wa polisi jamii.
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha ITV kimefika katika eneo la Nyamongo na kushuhudia baadhi ya nyumba
zinazodaiwa kubomolewa na kikundi hicho cha Saiga ambacho kilianzishwa
kwa nia njema na jeshi la polisi kanda maalum ya Tarime/Rorya katika
kukabiliana na vitendo vya uhalifu,yakiwemo matukio ya
mauaji,unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi, lakini kwa hivi sasa
kikundi hicho kimeacha majukumu yake ya msingi na kuamua kujichukulia
sheria mkononi ambapo watuhumiwa wa uhalifu huo wanasemekana kutorokea
nchi jirani ya Kenya.
Viongozi wa dini katika eneo hilo la North Mara wamelitaka jeshi la
polisi kuacha kufumbia macho vitendo vya kihalifu vinavyohatarisha
amani katika jamii kwa kisingizio cha mila kwani kundi hilo la Saiga
haliko juu ya sheria na pia hakuna mila inayoruhusu kikundi cha watu
kubomoa nyumba au duka la mtu na kuchukua samani za ndani, pesa au
bidhaa nyingine yoyote.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya naibu
kamishna Sweetbert Njewike,amekiri kuwepo kwa kikundi hicho ambacho pia
kinahusishwa na mauaji ya wakazi wawili wa Nyamongo na kuhaidi
kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika na
ubomoaji wa nyumba za wananchi kutokana na kujichukulia sheria mkononi.