Tunapoelekea kumaliza mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka mpya wa
2016, wananchi hutumia muda huo kwenda katika nyumba za ibada ama
kusherekea katika maeneo mbalimbali ya starehe, ambapo uzoefu unaonyesha
kuwa baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo
vinavyohatarisha usalama wa raia mali zao.
Jeshi la Polisi nchini,limejipanga vizuri katika mikoa yote kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha
kwamba vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza hususani katika
kipindi hiki cha kuelekea mkesha wa mwaka mpya vinadhibitiwa.
Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia,fukwe za bahari,
sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko
mikubwa ya watu.
Aidha,Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa
makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi
wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama
maeneo ya biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa
ni 111 au 112.
Pia, Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa
wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama
barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza
watu kupita kiasi, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga
honi hovyo.
Vilevile, wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabani pamoja
na kupiga mafataki. Aidha, yeyote atakayefanya vitendo hivyo hatua kali
za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nawatakieni watanzania wote kheri ya mwaka mpya.
Imetolewa na:Advera John Bulimba-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.