Watu watatu wamefariki baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kama
kivuko cha kusafirisha abiria kutoka ufukweni kwenda kwenye boti
ijulikanayo kama Mtu Ni Watu kuzama kwenye eneo la Mihama jijini
Mwanza.
Ajali hiyo imetokea majira ya saa tatu usiku wa kuamkia leo, ambapo
kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Kamishna msaidizi mwandamizi Justus
Kamugisha amethibisha kutokea kwa ajali hiyo
Takribani miaka ishirni tangu kuzama kwa meli ya MV
Bukoba kilometa chache tu kabla ya kutia nanga jijini Mwanza bado
mioyo ya watu ina simanzi kwa kuondokewa na wapendwa wao.
Yapo maelezo yasiyo na shaka kuwa baada ya baadhi ya abiria kuzuiwa
kupanda meli mjini Bukoba walitafuta usafiri wa barabara hadi Kemondo
ambapo waliingia kwenye meli na ilipopinduka na kuzama watu wengi
walipoteza maisha.
Hayo yamejitokeza tena jijini Mwanza Mwaloni Kirumba ambapo
wafanyakazi wa mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini
SUMATRA mbali na kuwazuia abiria waliotaka kusafiri na Boti ijulikananyo
kama Mtu Ni Watu toka jijini Mwanza kuelekea kisiwa cha Goziba wilaya
ya Muleba mkoani Kagera bado abiria hao walikodi pikipiki hadi ufukwe wa
Mihama kuisubiria boti hiyo bila ya kujali zuio la SUMATRA.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Justus Kamugisha
amesema tukio hilo ni matokeo ya kukaidi amri halali iliyowataka
wamiliki wa boti hiyo ya mizigo kutoitumia kusafirisha abiria.
Kwa mujibu wa maelezo ya manusura wa ajali hiyo
wamesema kuwa mtumbwi huo ulikuwa na abiria kumi idadi iliyokuwa
inatolewa ufukweni kwenda kwenye boti kubwa.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Rhobi Marwa mkazi wa Bunchali Tarime
mkoani Mara, Rehema Magoke aliyekuwa muuzaji wa Duka la dawa kisiwani
Goziba na Ismail Mazege mkazi wa Mihama jijini mwanza aliyekuwa nahodha
wa mtumbwi uliozama.