Lowassa kukinukisha Iringa Agosti 30

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa anatarajia kutimua vumbi katika jimbo la Iringa Mjini, Agosti 30 (Jumapili) endapo ratiba hiyo iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, haitabadilika.

Lowassa anayewania nafasi hiyo kupitia vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), atawasili mkoani Iringa siku moja tu baada ya umoja huo kufanya uzinduzi wa kampeni zake jijijini Dar es Salaam.

UKAWA wanatarajia kuzindua rasmi kampeni zao Agosti 29, katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam baada ya kuruhusiwa kuutumia uwanja huo ambao awali ulielezwa kutaka kutumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa shughuli nyingine.

Akizungumza na wanahabari hii leo, Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema tofauti iliyokuwepo imekwishamalizwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambao wamewapa ruhusa ya kuutumia uwanja huo.

“Baada ya ruksa hiyo, uzinduzi wa kampeni zetu upo pale pale, na utafanyika katika viwanja hivyo kuanzia saa 4.00 asubuhi Agosti 29,” alisema.

Akiwa mkoani Iringa Agosti 30, Lowassa atafanya mikutano katika majimbo mengine wilayani Mufindi, Kilolo na Iringa Vijijini kabla ya kuhutubia wakazi wa jimbo la Iringa Mjini ambalo kwa miaka mitano iliyopita limeongozwa na Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) anayewania tena nafasi hiyo.

Naye Mgombea Mwenza wa Lowassa, Juma Duni Haji anatarajiwa kufanya mikutano kama hiyo katika majimbo ya Mafinga Mjini, Mufindi Kaskazini, Mufindi Kusini, Kilolo, Isimani na Kalenga, Septemba 10.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza mgombea mwenza wa tiketi ya CCM akihutubia Jimbo la Arumeru.
Septemba 29 kwa mujibu wa ratiba hiyo, Mgombea Mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan  atafanya mikutano ya kampeni hizo za urais, ubunge na udiwani, Iringa Vijijini na Iringa Mjini huku Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Pombe Magufuli akitarajia kuungana na mgombea mwenza wake huyo kuushambulia mkoa wa Iringa, Septemba 30.

Wakati Dk Magufuli atafanya mikutano Iringa Vijijini na Mafinga Mjini, mgombea mwenza wake atafanya pia Iringa Vijijini na Mufindi kabla hajaelekea mkoani Njombe.

Oktoba 1 na 2, Dk Magufuli ataendelea na kampeni hizo mkoani Iringa kwa kufanya mikutano Iringa Vijijini, Kilolo na Iringa Mjini kabla hajaelekea mkoani Dodoma.

Oktoba 7 na Oktoba 20 itakuwa zamu ya UKAWA kutikisa mji wa Iringa kwa mara nyingine tena kwa mgombea mwenza wake kufanya mkutano mjini Iringa Oktoba 7 huku Lowassa akitarajiwa kurudi tena Oktoba 20.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo