SEHEMU ya gereza la King'ong'o linalopatikana karibu na Nyeri mjini iliteketea katika moto ulioanza usiku wa kuamkia Jumanne na kuwaacha walinzi 36 wa gereza bila makazi.
Jumla ya vitengo 36 vya makazi vilichomeka katika moto ambao walioshuhudia wamesema ulianza mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Jumanne.
Moto unaaminika kuanza katika nyumba moja iliyo katika sehemu ya chini na kuenea haraka, huku walinzi wakijibidiisha kuuzima na kujaribu kuokoa mali yao.
Hata hivyo, mali yao iliharibiwa na moto ule licha ya kikosi cha zimamoto Kaunti ya Nyeri na polisi kufika kwa haraka.
Juhudi zao zilzidiwa na ndimi zile za moto na mali yao ya thamani zaidi ya Shilingi 100,000 kuteketea.
Walinzi wa gereza ambao waliathirika walionekana wakipitia mabaki ya kile kilikuwa sare zao wakijaribu kuokoa baadhi ya bidhaa zao.
Akizungumza na Taifa Leo, Kamanda wa magereza wa eneo la kati, Hassan Bugu alisema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.
"Mali yenye thamani ya mamia ya maelfu iliharibiwa. Chanzo cha moto huo bado hakijatambuliwa kwa sasa lakini uchunguzi umeanzishwa," alisema Kamanda Bugu na kuongeza kuwa mbao zilizotumika kujenga nyumba zile ndizo zilifanya moto kuenea kwa kasi zaidi.
Makazi mbadala
Bw Bugu alisema kuwa maafisa walioathirika na familia zao watapewa vitengo vya muda vya makazi huku idara ya magereza ikiendesha mpango wa kuwapa makazi mapya.
"Tunahamasisha rasilimali zetu za kindani ili tuwape walinzi makazi ya muda lakini pia tunatoa wito kwa idara ya magereza ituunge katika kupatia familia hizi makazi mapya," alisema Bw Bugu.
Hakuna aliyejeruhiwa wakati wa tukio hilo.