Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili yao ya kazi bila kujali changamoto zinazowakabili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu oktoba 25 ili kuepusha machafuko.
Gallawa ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma kwenye mkutano wa wadau wa habari uliofanyika mjini Dodoma.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa amewataka waandishi wa habari kujiepusha na vitendo vya rushwa katika kampeni hizi za uchaguzi mkuu zinazoendelea kwani zinaweza kuwashushia heshima yao.
Amesema katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu kila mwananchi anategemea kupata taarifa sahihi za jinsi kampeni hizo zinavyoendelea kupitia vyombo vya habari na waandishi wa habari hivyo kama watazipotosha zinaweza kuleta madhara kwa Taifa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari kanda ya kati (CPC) habel Chidawali amewataka wadau wa habari mkoa wa Dodoma kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waandishi wa habari ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuihabarisha jamii bila vikwazo.