Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema amepata taarifa kwamba kuna njama zinaandaliwa kwa lengo la kumuangusha mgombea ubunge Jimbo la Mtama kwa tiketi ya chama hicho, Nape Nnauye.
Dk. Magufuli aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Alisema Nape anaandaliwa njama ili asipite katika kinyang’anyiro cha ubunge jimboni humo kwa sababu aliwataka baadhi ya wana-CCM wajivue gamba wakati chama hicho kikiwa katika mchakato wa kufanya mabadiliko.
Hata hivyo, Dk. Magufuli alisema Nape ni kiongozi mzuri ambaye endapo yeye (Dk. Magufuli), angekuwa na uwezo wa kumhamisha, angemhamishia kwenda kugombea katika jimbo lake la Chato.