Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CUF, chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA) jimbo la
Segerea, Julius Mtatiro, ameilalamikia Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kwa kulibakisha jina la Anatropia Theonest
wa Chadema kwenye karatasi ya mpiga kura wa jimbo lake,
wakati walishakubaliana amejitoa.
Mtatiro alizungumza, alipokwenda kutembelea
kituo cha kupigia kura cha Tabata, Kisiwani jana na kusema,
kuwepo kwa jina hilo kwenye karatasi ya mpiga kura, ni makosa
kwa sababu mgombea huyo alishajitoa.
"Uchaguzi unaendelea vizuri, lakini lipo tatizo moja lililojitokeza ambalo ni kuwepo kwa jina la
Anatropia Theonest kama mgombea wa Ubunge wa jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chadema wakati alishajitoa, hiyo inaweza kuwachanganya wapiga kura,"alisema Mtatiro.
Amesema, Theonest ni wa Chadema lakini Ukawa walishakubaliana kumsimamisha Mtatiro
kuwa mgombea wa jimbo hilo chini ya mwamvuli huo.