Polisi mkoani
Mwanza wametumia mabomu ya
machozi mapema leo kutawanya
watu wanaoaminika kuwa wafuasi
wa Chadema walioingia mitaani
kushangilia wakiamini wagombea
wao wanaongoza katika matokeo
ya awali.
Tukio hilo limetokea kwenye kituo cha kupigia kura cha Shule ya
Msingi Mlimani, eneo la Butimba, Ghana na Shule ya Msingi
Buzuluga kwenye majimbo ya Nyamagana na Ilemela.
Taarifa toka jijini humo zinasema kundi la watu waliokuwa vituoni
wakisubiri kubandikwa kwa matokeo hayo, lililipuka kwa shangwe,
nderemo na shamrashamra baada ya matokeo hayo kubandikwa na
wasimamizi wa uchaguzi wakiamini wagombea wao wanaongoza.
Mwandishi wetu aliyeko jijini Mwanza amesema polisi waliingilia
kati na kufyatua mabomu ya machozi kutawanya wafuasi hao.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, mgombea ubunge wa Chadema na
mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo la Nyamagana, Ezekiel
Wenje anachuana vikali na aliyekuwa Meya wa jiji la Mwanza,
Stanslaus Mabula wa CCM.
Katika jimbo la Ilemela, mbunge anayemaliza muda wake, Highness
Kiwia wa Chadema anatetea nafasi yake kwa kupambana na
mgombea wa CCM, Anjela Mabula.
Uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani umefanyika jana Oktoba 25,
mwaka huu ambapo takribani Watanzania milioni 22.7
wamejiandikisha kwenye daftari la kudumu kwa upande wa Tanzania
Bara huku kwa upande wa Zanzibar zaidi ya wapigakura laki tano
wamejiandikisha.