Watoto wa kati ya miaka miwili waandamana kupinga wenzao kubakwa

ZAIDI ya watoto 200 waliandamana Kamukunji wiki mbili zilizopita. Watoto hao kati ya miaka miwili na kumi waliandamana kutoka eneo la Biafra hadi kwa afisi ya Naibu Kamishna, Pumwani, wakitaka sauti yao kusikilizwa.
Wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa yameandikwa jumbe mbali mbali, ilidhiirika kwamba watoto hao wasichana kwa wavulana walikuwa wamechoshwa na kubakwa na kudhulumiwa kimapenzi.
Ujumbe ‘’Kinyago na Kanuku tumechoka kubakwa” unaweza kuonekana mfupi lakini ni mzito hasa kutoka kwa watoto wa umri mdogo kama hao.
Kinyago na Kanuku ni vitongoji duni vilivyo katika eneo la Biafra, Eneo Bunge la Kamukunji. Kulingana na maafisa wa watoto eneo hilo visa vya ubakaji wa watoto wachanga vinahofisha.
“Visa vya watoto kubakwa eneo hili ni vingi sana, wavulana wanalawitiwa pia. Mwezi uliopita nilikuwa na kisa cha ubakaji kwa mtoto wa miaka miwili na mwingine wa miaka mitatu,” alisema Bi Mary Mugwe, Mwenyekiti wa kitongoji duni cha Kanuku.
Taifa Leo iliamua kutembelea vijiji hivyo kung’amua hali ilivyo. Kinachojitokeza mara unapoingia ndani ya kijiji ni uchochole.
Vijia vyembamba, maji machafu ya mitaro na giza ni picha unayokumbana nayo ndani ya kijiji cha Kanuku. Vijia ni vyembamba kiasi kwamba watu wawili hawawezi kuandamana mkabala na inabidi kufuatana unyo unyo.
Nyumbani mwa mmoja wa wakazi tunapatana na msichana wa umri mdogo akifua nguo nje ya nyumba yao ya chumba kimoja.  Tunapatana na mama wa msichana huyo ambaye hatutataja jina lake. Anatueleza kisa cha ubakaji dhidi ya msichana wake wa miaka 10.
Ni miaka miwili kamili tangu kitendo hicho kumfanyikia bintiye aliyekuwa na miaka minane wakati huo. Ni kitendo kilichomwacha mtoto huyo na majeraha mwilini na moyoni baada ya kushtuka sana.
Kufikia sasa mtoto huyo japo alitibiwa hospitalini na hupewa ushauri wa kila mara bado anahofu nyingi kwani kulingana na mamake, alitatizika ki akili.Mshukiwa alikamatwa na kufunguliwa mashtaka na kesi yake inaendelea alieleza mama huyo.
“Nilikuwa nimetoka nyumbani eneo la mashambani na watoto wangu wawili (msichana na mvulana) mwendo wa saa kumi na moja asubuhi. Tulipofika kijijini niliwaacha kidogo nikamwite ndugu yao ili anisaidie kubeba mzigo niliyokuwa nayo,” alianza kuhadithia.
Ni wakati huu ambapo kijana mmoja aliyekuwa akimfahamu alichukua fursa ya kuwatorosha watoto wake. Aliporudi mahali walipokuwa hakuwapata. Aliulizia lakini hakuna aliyemfahamisha walikokuwa wameenda.
Alipiga nduru, ndiposa watu waliokuwa wakienda kazini asubuhi wakakimbia kumsaidia, “Tulipowapata, binti yangu tayari alikuwa amebakwa,” alieleza mama huyo kwa huzuni.
Alielezea kuwa mbakaji alimtolea bunduki mvulana wake mdogo na kutishia kumuua ikiwa angesema alichoshuhudia.
Hawakuweza kumkamata wakati huo kwani alitoroka lakini kutokana na hali kwamba walikuwa wakimfahamu, alikamatwa baadaye.
“Kutoka wakati huo watoto wangu hawajawa na amani. Waliathirika sana kiakili. Siwezi kuwatuma nje kwa sababu huwa wanaogopa sana,” alieleza.
Msichana huyo hapendi kuona wanaume na humbidi mamake kumsindikiza hadi shuleni na kumwendea tena, alieleza.
Hawezi kwenda hata dukani ikiwa kuna mwanamume mbele yake, “Akiona mwanamume huwa anatupa pesa na kurudi kwa nyumba mbio akisema ameona mtu,” alieleza mama huyo.
Wakati wa usiku huwa hawezi kulala, “Nyakati zingine huwa anapiga nduru na kusema ameona mwanamume aliyemdhulumu. Huwa anashtuka mara kwa mara na kufikia sasa, bado anahisi uchungu.”
Ni kimoja kati ya visa vingi vya ubakaji, dhuluma za kimapenzi na ulawiti wa watoto katika vitongoji duni hivyo.
Mita chache kutoka kwa nyumba hiyo, kisa kingine, mtoto wa miaka mitatu alikamatwa na mbakaji miezi kadhaa iliyopita, “Tunashukuru Mungu kwa sababu wakati tulipofika alipokuwa hakuwa amemchafua ila alikuwa amemlalia mtoto wangu,” alieleza baba wa mtoto huyo.
“Sikuamini macho yangu, nilimkamata, tukapigana ila alinishinda nguvu na kutoroka. Lakini hakuenda mbali kwa sababu alikamatwa kwa sababu nilipiga nduru,” alieleza.
Alimpeleka mtoto hospitalini na mshukiwa alipelekwa moja kwa moja hadi kituo cha polisi, “Kisa hicho kinamsumbua sana kwa sababu kutoka wakati huo hadi sasa huogopa watu,” alieleza baba huyo.
Mshukiwa alifunguliwa mashtaka na kesi inaendelea ilhali mtoto anaendelea kupata ushauri, “Serikali inafaa kuwaadhibu vikali zaidi watu kama hao.”
Angekuwa na uwezo wa kifedha angemwamisha mtoto huyo kutoka eneo hilo. Kulingana na maafisa wa watoto eneo hilo, watoto wasichana kwa wavulana hawana usalama kutokana na visa vingi vya ubakaji na dhuluma vya kimapenzi.
Bw Kennedy Maina ni mmoja wa maafisa wa kujitolea wa watoto (VCO) katika mtaa Biafra na anaeleza kwamba kila mwezi mtoto mmoja au wawili hubakwa au kulawitiwa Kanuku na Kinyago.
“Hali ni mbaya sana, wasichana wamebakwa na wavulana wamelawitiwa. Watoto wa miaka miwili wamebakwa au kulawitiwa. Ingawa baadhi ya washukiwa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, baadhi yao wametoroka,” alisema wakati wa mahojiano.
Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, watoto wawili wa miaka mitatu wamedhulumiwa. Jambo la kuhuzunisha sana ni kwamba msichana mmoja kati yao aliambukizwa virusi vya Ukimwi na mshukiwa aliyetoroka, alieleza Bw Maina.
Anaeleza kwamba watoto wanaodhulumiwa ni kati ya miaka miwili na miaka 15, “Hata kina mama wananajisiwa. Tunaomba kupata msaada wowote kukomesha uhalifu huu. Wabakaji ni watu wanaofahamika katika jamii. Wengine huwa ni wezi,” alisema.
Wavulana nao walawitiwa
Afisa huyo alieleza kuwa takriban watoto 14 wavulana wamelawitiwa na mtu wanayemfahamu katika jamii. Mshukiwa huyo alikamatwa na kesi yake inaendelea mahakamani.
“Ni suala la kusikitisha sana. Tumeripoti kwa polisi mpaka hata wamechoshwa na ripoti hizo kwani limekuwa ni kama jambo la kawaida,” alisema afisa wa watoto Eneo Bunge la Kamukunji Bi Margaret Kagwiria.
Alieleza kuwa baadhi ya visa vya dhuluma dhidi ya watoto husababishwa na wazazi ingawa umaskini na ukosefu wa ajira kwa vijana wa eneo hilo umechangia sana.
Alisema baadhi ya wazazi husikizana na washukiwa, “Baadhi yao hulipwa ili kukomesha kesi. Katika kisa kimoja mama mmoja alikana kuchafuliwa kwa msichana wake,” alisema afisa huyo.
Alisema baadhi ya wazazi wamewaingiza watoto ndani ukahaba, “Wazazi huwa wanapewa Sh3, 000 au Sh4, 000 baada ya watoto wao kudhulumiwa kimapenzi ili kukomesha mashtaka. Kuna mama mmoja alimficha mtoto wake baada ya mtoto huyo kubakwa,” alidai Bi Kagwiria.
Bi Mugwe anaeleza kwamba katika kisa kimoja, mzazi wa mtoto mmoja aliyebakwa mara tatu, na mtu aliyemfahamu, alimtorosha mtoto huyo baada ya kuzomewa na wanakijiji kwa kusikizana na mbakaji wa mtoto huyo.
“Inakuwa vigumu sana kufuata kesi kama hiyo kwa sababu mtoto hayuko na mama hataki kushiriki. Hili sio suala rahisi kwa sababu watoto wanazidi kuharibiwa katika jamii kila siku,” alisema Bi Mugwe.
Bi Kagwiria alieleza tayari wameanzisha kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusiana na ubakaji, jinsi ya kuwakinga watoto wao. Alionya wazazi dhidi ya kuwakinga wabakaji wanaowajua.
Lakini sio hilo pekee, watoto wameingilia ukahaba, alieleza na kuongeza kuwa hali ni mbaya sana kwani watoto wanaoshiriki ukahaba wamewaingiza wengine katika biashara hiyo ya ngono eneo hilo.
“Inasikitisha kwamba wazazi wanawauza watoto wao katika ukahaba ili kujikimu kimaisha. Kuna shida kubwa sana na sijui hali itakavyokuwa siku zijazo,” alisema Bi Kagwiria.
Bi Saumu Saidi pia ni afisa wa kujitolea wa watoto (VCO) Kamukunji. Alieleza watoto wa chekechea na darasa la kwanza wanaelewa ngono katika vitongoji hivyo.
“Huwa wanaonyeshwa filamu chafu na wanambiwa kufanya walichoona ndani ya filamu hizo. Huwa wanapewa peremende ili kushiriki vitendo hivyo,” alisema Bi Saidi.
Alieleza kuwa watoto kutoka darasa la tatu na nne hufunzwa jinsi ya kushiriki mapenzi na hushiriki mapenzi wao kwa wao, “Wanaelewa kabisa,” alisema afisa huyo.
Huku baadhi ya wazazi wakiwa na ufahamu wa kinachoendelea, alisema wengine hawajui kwani huondoka mapema kwenda kazini na kurudi usiku sana.
Kulingana na Bi Saidi, ndani ya kijiji hicho kuna mwanamke atoaye mafunzo hayo kwa watoto, “Nilikabiliana naye siku moja. Aligeuka mkali sana kwangu,” alisema na kuongeza baada ya majibizano mwanamke huyo alikinga nyumba atekelezeayo maovu hayo.
Kulingana na wakazi, watoto walioathirika wanafaa kuondolewa eneo hilo ila wazazi tuliowahoji walisema hawakuwa na uwezo wa kuwahamishia watoto hao kwa mitaa bora.
Mwakilishi maalum wa eneo hilo Bi Zulfa Hakim alilaani vitendo hivyo na kuwataka wakazi kuwa makini kuwakinga watoto wao dhidi ya wabakaji.
Mbunge wa Kamukunji Bw Yusuf Hassan pia alisema alikuwa na ufahamu kuhusiana na uhalifu huo. Kupitia kwa msaidizi wake alisema, “Tunatia juhudi kukomesha ubakaji. Baadhi ya washukiwa tayari wamekamatwa na wamefunguliwa mashtaka.”
Sheria dhidi ya dhuluma za kimapenzi kwa watoto
MTOTO ni mtu yeyote ambaye hajafikisha umri wa miaka 18 kulingana na sheria ya watoto.
Sheria kuhusiana na ubakaji nchini ni kali sana na washukiwa wa ubakaji hutazamia miaka isiyopungua 10 wakithibitishwa kuhusika katika kitendo hicho.
Kulingana na sheria, mtu yeyote anayethibitishwa kumbaka mtoto wa miaka 11 na chini anafaa kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Sheria hiyo inaeleza kuwa mtuhumiwa wa ubakaji wa mtoto kati ya miaka 12 na 15 hutazamia kifungo kisichopungua miaka 20 gerezani akithibitishwa kuhusika.
Na adhabu ya mbakaji wa mtoto kati ya miaka 16 na 18 hutazamia kifungo cha miaka isiyopungua 15 akithibitishwa kuhusika.
Sheria hiyo inaeleza kwamba mshukiwa aliyejaribu kubaka hutazamia hukumu ya miaka isiyopungua 10 gerezani.

Kuwakinga dhidi ya kuingizwa kwa ukahaba
Sheria pia imewakinga watoto dhidi ya kuingizwa katika ukahaba, kuona filamu chafu au dhuluma za kimapenzi.
Sheria hiyo iliwekwa kukinga watoto na kuimarisha maisha yao nchini. Inazungumzia adhabu kwa wabakaji wa watu wazima pia.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo