Wananchi wa vijiji vya Kituri na Kifaru wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wamelazimika kuchukua hatua za kusafisha mto Ruvu kwa kuondoa Magugu maji,magogo na tope kwa kutumia Ngalawa na Trekta ili kunusuru mto huo ambao uko hatarini kukauka.
Akizungumza wakati wa zoezi la kusafisha mto huo mkurugenzi wa shirika la mazingira na utalii Tanzania (TETEO) Bw.Ally Makiade amesema hali ya mto huo kwa sasa ni mbaya kutokana na kushamiri kwa vitendo vya uharibifu wa Mazingira
Amesema zoezi la kuondoa uchafu katika mto huo ni gumu kutokana na ukosefu wa vifaa kwa madai kuwa kuna magogo makumbwa ambayo yanahitaji katapila na kwamba zoezi hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kunusu mto huo ambao unategemewa kwa kiasi kikubwa na wananchi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake mhandisi wa mazingira anayesimamia raslimalii za maji kutoka bonde la pangani Bi.Arafa Majid amewataka wadau mbalimbali kujitolea kusafisha mto huo kwa kuwa maji mengi yanapotea kutokana na mto huo kujaa uchafu na magugu maji ambayo kama hayataondolewa mapema kuna hatari ya maji kukauka kabisa.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mwanga ambao wamejitokeza kusafisha mto huo wamesema hali ya mto huo kwa sasa ni mbaya kutokana na maji kuanza kupungua kwa kasi ikilinganisha na miaka kumi iliyopita na kwamba wananchi wa wilaya hiyo wanategemea maji ya mto huo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na umwagiliaji.
