Mgombea mwenza wa urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Mh. Juma Duni Haji amefanya mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu katika majimbo ya mkoa wa Dar es Salaam na kuhaidi kuboresha huduma za kijamii pamoja na miundombinu ya jiji hilo ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaosababishwa na uchafu kwa kuhakikisha huduma ya maji inakuwa endelevu na ya uhakika wakati wote.
Mgombea mwenza huyo wa Chadema, Mh. Juma Haji Duni anayewakilisha vyama vinavyunda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA, ameanzia mikutano yake katika jimbo la Segerea, ambako ametumia wasaa huo kunadi sera na ilani ya chama hicho huku akiwasihi watanzania kumpigia kura nyingi za ndiyo mgombea urais wa Chadema Mh. Edward Lowassa ili kumaliza kero ya maji jijini na tatizo la uchafu katika jiji hili ambalo ni mji mkuu wa Tanzania.
Baada ya kuhutubia wakazi wa jimbo la Segerea na kisha kuelekea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julius Nyerere kuelekea unguja kushiriki mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya UKAWA, Maalim Seif Sharif Hamad, kijiti cha mbio hizo kikadakwa na makamu mwenyekiti wa Chadema taifa kutoka Zanzibar Said Issa Mohamed ambaye amemuombea kura Mh. Edward Lowassa katika mikutano iliyofanyika kwenye viwanja vya mwembe yanga, Temeke na Kigamboni.