Polisi mkoani Geita imefanikiwa kuokoa baa moja maarufu iliyopo mkoani humu (jina limehifadhiwa) isiteketezwe na moto na wananchi wenye hasira waliokuwa wakidai inahusika na matukio ya vifo vya kutatanisha vya walinzi watatu waliofariki dunia kwa nyakati tofauti.
Wananchi hao walikuwa na hasira ya kutaka kuteketeza baa hiyo baada ya walinzi hao (majina yao yamehifadhiwa), wakazi wa mkoani Geita, kufariki dunia ikiwa ni miezi minne tangu mlinzi mwingine kuuawa akiwa lindoni.
Vifo hivyo viliwafanya wananchi waamini kwamba vinatokana na imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo (pichani), alisema tukio hilo limewafanya wananchi kuhusisha na imani za kishirikina lakini polisi wanaendelea kulifanyia uchunguzi kitaalam.
‘’Upelelezi umefikia hatua nzuri, tupo hatua nzuri ya kuwanasa watuhumiwa waliotaka kuhusika na tukio hilo, lakini tunafanya hivyo kwa kuzingatia sheria kwani matukio hayo yameacha utata mkubwa,” alisema Kamanda Konyo.
Alisema baa hiyo kwa sasa imefungwa kutokana na shinikizo la wananchi na pia mmiliki wake huenda anahofia usalama wake huku akiwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi.
Hata hivyo, Mchungaji Samson Mkamato, wa Kanisa la Muungano wa Makanisa ya Kipentekoste mkoani humu, alisema anasikitishwa na hatua hiyo kutokana na watu wengi kuweka mbele imani za kishirikina na kupoteza hofu ya Mungu.
“Ninashauri ulinzi shirikishi kuimarishwa na kuna haja ya viongozi wa dini kuelimisha jamii ili kuepukana na imani za kishirikina kama ambavyo wananchi walivyopandwa hasira kutokana na vifo vya walinzi hao,” alisema Mchungaji Mkamato.