Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, mhe. William Lukuvi ameiagiza halmashauri ya jiji la Mbeya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watendaji wa idara ya ardhi ambao waliingiza malipo hewa ya fidia katika mradi wa upimaji viwanja wa Sisitila kwa madai kuwa walikuwa na nia mbaya ya kuiingizia serikali hasara.
Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi,Mh.William Lukuvi amefanya ziara jijini Mbeya na Kutembelea maeneo yenye migogoro ya ardhi na akiwa kwenye mradi wa upimaji wa viwanja wa Sisitla unaoendeshwa na halmashauri ya jiji la Mbeya akaelezwa tatizo la uwepo wa malipo hewa kwenye mradi huo.
Akizungumzia madai ya wananchi hao mbele ya waziri Lukuvi, kaimu mkurugenzi wa jiji la Mbeya,Dk.Samwel Lazaro amekiri kuwepo na tatizo la malipo hewa kwenye mradi huo, lakini akadai kuwa wahusika walishachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi.
Baada ya kusikiliza kilio cha wananchi na majibu ya halmashauri,waziri Lukuvi akasema hatua ya baadhi ya watendaji hao kufukuzwa kazi haitoshi na akaagiza wote walioshiriki kukamatwa na kufikishwa mahakamani.