Wanachama wa CCM na Chadema wa familia mbili tofauti wamepigana na kuumizana vibaya wakizozana kuhama katika vyama hivyo.
Mkasa huo ulitokea juzi katika Kijiji cha Nondo Wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa baada ya Wagombea Udiwani wa CCM kumaliza kikao chao, wakiwaomba wanachama wenzao wawachague katika kura ya maoni.
Ugomvi huo ulihusisha familia ya Katibu Mwenezi wa CCM wa kata hiyo, Meidi Sinkambana mwanawe Hamoud Milambo na familia ya mwanachama wa CHADEMA, Waton Silawena mwanawe Megji Silawe.
Ilidaiwa kuwa Megji alianza kumshambulia kwa maneno Katibu huyo Mwenezi wa CCM akihoji kwa nini amewaleta madiwani hao wa CCM kujinadi kijijini kwao wakati wanachama wa CHADEMA wakifurahia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassakujiunga rasmi na chama hicho.
Malumbano hayo ya maneno yalimkasirisha Hamoud ambaye aliingilia kati ili kumsaidia mama yake mzazi huku Mzee Kasomo naye akimtetea mwanawe Megji.

