LOWASSA Asema anahitaji Kura Milioni 10 tu ili Awe Rais wa Tanzania


Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa amesema kama Watanzania watashindwa kufanya mabadiliko kwa kupiga kura kuing’oa CCM madarakani mwaka huu, hawataweza kufanya hivyo tena, huku akihoji kama vyama tawala mbalimbali katika nchi za bara la Afrika vimeng’oka madarakani: “Kwa nini isiwe CCM”.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni katika Uwanja wa Gangilonga Iringa Mjini uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji huo, Lowassa aliyeambatana na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alisema vyama tawala vilivyokuwa rafiki na CCM vimeshang’oka madarakani na kwamba hivi sasa ni zamu ya chama hicho tawala kuondolewa.

“Nataka kura nyingi ili hata wakiiba tushinde, asilimia 90 ziwe zetu hizo 10 waache waibe. Msipoiondoa CCM mwaka huu hatutaiondoa tena, CCM na Tanu walikuwa na marafiki zao lakini karibu wote wameondoka.

“Chama cha Kanu cha nchini Kenya kimeshaondoka madarakani, kile cha Malawi (Malawi Congress Party) nacho kimeondoka, UNIP (The United National Independence Party cha Zambia) nacho imeondoka na kile chama cha Mzee Obote (Dk Militon) cha Uganda kimeondoka, tunaona pia jinsi Rais wa Zimbabwe (Robert Mugabe) anavyohangaika,”alisema Lowassa.

Katika mkutano huo, Lowassa alirudia vipaumbele vya ilani ya uchaguzi ya Ukawa, huku akimponda mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM, Frederick Mwakalebela kuwa hawezi kushinda kwa maelezo kuwa amepanda gari bovu.

Sumaye alieleza ufisadi mbalimbali uliotokea tangu Lowassa alipojiuzulu mwaka 2008, huku akihoji yalipo majina ya wauza dawa za kulevya na majangili ambayo alidai kwa nyakati tofauti Rais Jakaya Kikwete amenukuliwa akisema kuwa anayo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi ambao walianza kufika uwanjani saa nne asubuhi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo. 
 
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo saa 11.58 jioni, baadhi ya wananchi hao walilisukuma gari la Lowassa na mgombea ubunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chadema, Mchungaji Peter Msigwa hadi katikati ya mji huo kabla ya magari hayo kushika kasi na kuwaacha wakiendelea kukimbia barabarani huku wakiimba nyimbo mbalimbali.

Baadhi yao walionekana kubeba kitu mfano wa jeneza na kukivisha bendera ya CCM huku wakisema mwisho wa chama hicho tawala ni Oktoba 25.

Aomba kura milioni 10
Akiwa Mafinga Mjini, Lowassa alisema anahitaji Watanzania wampigie kura si chini ya milioni 10.2 ili awe rais na kumaliza kilio cha wakulima nchini.

Akiwa katika siku ya kwanza ya kampeni zake mikoani hapa, Lowassa aliwaeleza wananchi wa Mafinga kuwa amechoshwa na manyanyaso ambayo wakulima wanaendelea kuyapata ikiwamo kukopwa mazao yao na kutozwa ushuru na Serikali bila ya wao kupata faida yoyote.

Lowassa alisema mara atakapochaguliwa kuongoza nchi, kitu kikubwa atakachokifanya kuwasaidia wakulima ni kufuta ushuru wote wa mazao na kuhakikisha wananufaika na jasho wanalolitoa wakati wa kilimo.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Wambi, Mjini Mafinga, Lowassa alisema: “Nakataa wakulima kuendelea kukopwa mazao yao na kutozwa ushuru, kuendelea kufanya hivi ni kuwanyonya na kutaka waendelee kuwa maskini wakati wao wanafanya kazi kwa kujituma sana.”

Alisema hayo yatafanyika iwapo wananchi watampigia kura za kutosha na kuzilinda huku akigusia madai kwamba CCM ni wezi wa kura na kubainisha kuwa maneno hayo si ya kubeza wala kuyafumbia macho.

“Mimi nataka kila mtu akihifadhi vizuri kichinjio chake (kadi ya kupigia kura) na siku ya kupiga kura ikifika nawaomba wanawake kwa wanaume wajitokeze kwenda kupiga kura ila kina baba ninawaomba mkishapiga kura fanyeni kazi ya kuzilinda kura zenu,” alisema Lowassa na kuongeza: “Kweli CCM ni wajanja sana kazi tunayotakiwa kufanya ni kuziba mianya yote, hata kama tukipigwa chenga wawe wamepata asilimia 10 ili asilimia 90 zibaki kwetu.”


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo