ACT - Wazalendo: Waziri Mkuu Atakuwa Zitto Kabwe

CHAMA cha ACT Wazalendo kimezindua kampeni zake jijini Dar es Salaam kwa kuahidi kitakapopewa ridhaa ya kuongoza nchi, kitaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Aidha katika uzinduzi huo ambao viongozi mbalimbali wa chama hicho walihutubia, Mgombea Urais wa chama hicho Anna Mghwira alisema wananchi wakimpa ridhaa, waziri mkuu wake atakuwa Zitto Kabwe.

“Nitakapounda serikali, katika katiba, mtu wa kwanza kusaidiana na rais licha ya makamu, ni Zitto Kabwe, atakuwa Waziri Mkuu katika serikali ya kwanza,” alisema Anna Mghwira ambaye pia alisema atahusisha viongozi waadilifu kutoka CCM, Chadema na vyama vyote vya siasa na taasisi zote kiraia.

Akihutubia mkutano huo uliofanyika viwanja vya Mbagala Zakhem, mgombea huyo, katika kuelekeza nia yake ya kuunda serikali hiyo ya umoja, alisema linapokuja suala la kitaifa, hakuna haja ya kuangalia masuala ya itikadi.
 
 “Mimi ni mama, hukusanya watoto wake.Hata mama wa vifaranga hukusanya vifaranga pamoja na kuviweka kwenye mbawa zake…mimi nina mbawa za moyo…nitaunda serikali ya umoja wa kitaifa itakayotokana na sekta binafsi lakini kutoka watu wazalendo, wenye utu, waadilifu, taasisi za kijamii, mashirika ya kidini, makundi ya umma ili kuunda taswira ya nchi yetu.”

Mghwira alisema taifa linahitaji mabadiliko si ya tu kifikra na kisera, bali pia ya kijinsia kwa kumchagua yeye kuwa Rais wa nchi. Alisema chama chake kinatilia mkazo utu, uzalendo na uadilifu.

Makao makuu Dodoma 
Aidha alisema, Serikali itakapoundwa itaapishwa Dodoma na watahakikisha wanarudisha kazi kubwa aliyoifanya Rais wa Kwanza, Julius Nyerere ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na serikali lakini siyo makao makuu ya chama.

Alisema kuweka mji huo makao makuu, maana yake ni kuleta watu wote kutoka pande zote za nchi.
 
Vipaumbele 
Alitaja vipaumbele vyake ni kuwa na mfumo imara na endelevu wa hifadhi ya jamii unaojengea uwezo wananchi kukabiliana na majanga. Alisema asilimia sita pekee ya Watanzania wanafaidika.

“Tutatumia hifadhi ya jamii kama nyenzo ya kukuza akiba nchini ili kuwe na vyanzo vya mitaji ya uwekezaji wa ndani…tutapanua hifadhi ya jamii kufikia makundi yote katika jamii ikiwamo wakulima, wafugaji, mama lishe na bodaboda,” alisema. 
 
Kipaumbele kingine alichoahidi ni uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora.

Alisema watu wengi hawana uhakika na maisha yao kimapato. Aidha alisema, watajikita kwenye uwekezaji wa kilimo na kusimamia uzalishaji wake.
 
 Aidha, aliahidi kuhakikisha ardhi na mashamba yote yaliyo chini ya mashirika ya umma, yanachukuliwa na kuwekwa chini ya uzalishaji mdogo.

Kwa upande wa viwanda, alisema atahakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinaongeza mapato ya fedha za kigeni. 
 
Chama hicho kupitia kwa mgombea, kimesema kitaweka msukumo kwenye bidhaa za nguo na vitakuwapo viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo.

Vipaumbele vingine ni kuhakikisha madini, mafuta na gesi, vinakuwa mali ya wananchi kikatiba. 
 
Kuhusu Katiba Mpya, alisema wataruhusu Tume ya Jaji Warioba imalize kazi ya katiba ilikoishia. Mgombea huyo aliendelea kutaja vipambele vyake kuhakikisha anaboresha huduma za afya ikiwamo kudhibiti vifo vya mama na mtoto.

Aliahidi kuondoa tatizo la watoto wa mitaani. Misamaha ya kodi kwa mujibu wake, haitazidi asilimia moja ya pato la taifa na wakati huo huo atadhibiti mianya ya ukwepaji kodi hususani kwa kampuni za kigeni.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo