Rais wa Msumbiji Filipe Nyussi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi amesema kamwe taifa lake haliwezi kusahau mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania katika harakati zake za kuikomboa nchi hiyo kutoka katika mikono ya wakoloni na hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yake inafurahia matunda ya uhuru walionayo kwa kuwa na utawala wa kidemokrasia.
Mh Nyussi ameyasema hayo alipotembelea chuo cha diplomasia na kuzungumza na wanafunzi na vionozi wa chuo hicho ambapo amesema katika eneo lilojengwa chuo hicho ndipo yalikuwa makao makuu ya chama cha Frelimo kilichokuwa kikitumika kudai uhuru wa nchi hiyo na sasa wanafaidi matunda ya utawala wa kisheria.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho balozi Mwanaidi Majaar amesema jambo la msingi ni watu kukumbuka historia za nchi zao ili kuweza kujua walipo na wapi wanakwendana hasa katika mtizamo wa kiafrika zaidi.
Awali rais huyo alipata nafasi ya kukutana na wafanyabishara ambapo amesema uchumi wa nchi yake umeweza kukua kwa zaidi ya asilimia saba kwa mwaka jana kutokana na uwekezaji kutoka nje ambapo katika mkutano huo pia ulihudhuriwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu uwekezaji na uwezeshaji injinia Chirtopher Chiza ambaye amewataka wafanyabiashra wa Tanzania kwenda kuwekeza Msumbuji.