Na Hassan
Silayo na Lorietha Laurence
RAIS wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete anatarajia kufungua mkutano
wa Kilimo wa Umoja wa Nchi za Kusini mwa Africa, utakaofanyika tarehe 13 hadi
14 Mei mwaka huu .
Hayo
yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkutano wa Vyama vya Kilimo vya Kusini
mwa Afrika (SACAU), Ishmael Sunga wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu
mkutano huo utakao fanyika katika hoteli ya White sands iliyopo jijini Dar es
salaam.
Alisema kuwa
kipaumbele katika kipindi hiki ni kupambana na changamoto ya kilimo,na usalama
wa chakula ili kufanya sekta ya kilimo kukua , kustawi na kufanya kilimo kuwa
biashara badala ya kufikiri katika kuondoa umaskini.
“Lengo litakuwa ni kubadilisha mtazamo wa watu
kuwa, kilimo ni kwa ajili ya kumfanya mkulima ajikimu mahitaji ya kawaida na
kuondoa umaskini, bali ni kumfanya mkulima kupata faida na kutajirika kupitia
kilimo katika ngazi zote za kilimo”, alisema Sangu.
Aliongeza
kuwa mkutano huo una malengo ya kuwasaidia na kuwaongezea nguvu wakulima pamoja
na kutoa taarifa za kilimo kwa wadau wa sekta hiyo kwa niaba ya wakulima wote
wanachama wa umoja huo ili kuleta tija katika sekta hiyo muhimu ya kilimo.
Naye Mkurugenzi
wa Baraza la Kilimo Tanzania Janet Bitegeko alisema baada ya mkutano huo
washiriki watapata fursa ya kutembelea wakulima wa mpunga katika kijiji cha Bagamoyo
ili kujionea changamoto na nini wakulima hao wanafanya na kutoa ushauri ili
kuweza kuboresha zaidi zao hilo.
Janet
aliongeza kuwa umoja huo utatoa taarifa za utekelezaji za mwaka pamoja na
kufanya ukaguzi wa hesabu za mwaka za umoja huo.
Mkutano huo
utahudhuriwa na washiriki kutoka nchi 14 wakiwemo wakurugenzi na wenyeviti
kutoka nchi za kusini mwa afrika, wawakilishi zaidi ya 10 wa muungano wa wakulima
pamoja na taasisi za kifedha.
Kauli mbiu
ya mkutano huo ni kusaidia kilimo cha biashara na maendeleo ya biashara
yanayolenga mkakati maendeleo ya kilimo katika nchi za kusini mwa afrika,
ambapo waziri wa kilimo wa Nigeria atatoa kauli.