Licha ya mvua za masika kuendelea kunyesha kwa wingi wilayani Makete mkoani Njombe na kupelekea barabara nyingi za kuelekea kwenye vijiji mbalimbali kutopitika kirahisi, zoezi la wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura linaendelea vizuri
Mwandishi wa mtandao huu ameshuhudia magari yanayopeleka vifaa hivyo kupita kwa tabu kwenye barabara zenye tope, huku kwenye vijiji vingine mashine za kuandikisha wapiga kura (za BVR) zikipelekwa kwa pikipiki
Akizungumza na mtandao huu wa eddymoblaze.blogspot.com Afisa Uchaguzi msaidizi wilaya ya Makete Bw. Gregory Emmanuel amethibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo na kudai kuwa wamejitahidi kuhakikisha vifaa vyote vimefika katika kila kituo
Amesema katika vijiji vingine vifaa vimefika asubuhi ya leo 03 Aprili (siku ya kuanza uandikishaji kwa vituo vya awamu ya tatu/kanda ya tatu) kutokana na uharibifu wa barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani hapa
"Kuna maeneo mengine hata wale operators (waendesha mashine) wa BVR wamefika leo asubuhi na wamefikishwa kwa usafiri wa pikipiki na wengine wametembea kwa miguu" amesema Bw. Gregory
Bw. Gregory amevitaja vijiji vilivyokuwa na changamoto ya miundombinu kuwa ni Unyangogo katika kata ya Iniho, baadhi ya vijiji vya kata ya Kipagalo, Makwaranga na Makeve katika kata ya Ipelele na kusema kuwa usambazaji wa vifaa katika maeneo hayo umefanyika kwa tabu kubwa
Wakati mtaalamu wa mashine za BVR akiwa njiani akielekea katika kituo cha Unyangogo katika kata ya Iniho, alianguka na pikipiki japo hakuumia, lakini pikipiki iliumia pamoja na dereva kupata michubuko kidogo
Pamoja na changamoto zote imeelezwa kuwa zoezi hilo bado limefanyika kwa ufanisi na wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
Zoezi hilo linaendelea kwa awamu ya tatu (kanda ya tatu) katika kata za Kipagalo, Bulongwa, Luwumbu, Iniho na Ipelele ambapo zoezi hilo limeanza Aprili 03 na linatarajiwa kumalizika katika kata hizo Aprili 09 mwaka huu.
Na Edwin Moshi