Mkazi wa Uyole katika Jiji la Mbeya, John Benedict maarufu Dk Bony (43) amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akituhumiwa kutapeli wagonjwa kwa kujifanya daktari bingwa wa upasuaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Novemba 27, mwaka huu saa 7:00 mchana, Benedict alikamatwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Askari polisi kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali hiyo walimkamata mkazi huyo wa Uyole kwa tuhuma za kujifanya mtumishi wa serikali kama daktari wa upasuaji katika hospitali hiyo.
Alisema inadaiwa chanzo ni kuwatapeli ndugu wa wagonjwa ili kujipatia kipato kwa njia isiyo halali.
Mtuhumiwa alikamatwa na wananchi waliokuwepo hospitalini hapo na kuokolewa na walinzi wa hospitali kabla ya polisi kufika.
Aidha, mtuhumiwa alilazwa hospitalini hapo kutokana na kuumia miguuni. Mkuu wa mkoa alisema Novemba 28, mwaka huu saa 10:50 jioni mtuhumiwa Benedict alifariki dunia.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi wa kitabibu.