Vijana nchini Ufaransa watapata kondomu bila malipo kuanzia Januari, katika jitihada za kupunguza kuenea kwa magonjwa ya zinaa (STIs).
Rais wa Ufaransa alitangaza hatua hiyo mpya ya afya siku ya Alhamisi katika hafla ya afya ya vijana.
Emmanuel Macron alisema vijana wataweza kuzikusanya kutoka kwa maduka ya dawa, na akaelezea hatua hiyo kama "mapinduzi madogo ya uzazi wa mpango".
Mnamo 2020 na 2021 Ufaransa ilipata ongezeko la 30% la viwango vya magonjwa ya ngono kitaifa. Hatua hiyo mpya inakuja pamoja na mipango mingine ya afya inayolenga kuenea kwa magonjwa ya zinaa na kuboresha upatikanaji wa uzazi wa mpango.
Mnamo mwaka wa 2018 serikali ya Ufaransa ilianza kurejesha gharama za kondomu kwa watu binafsi, ikiwa zilinunuliwa katika duka la dawa kwa maagizo kutoka kwa daktari au mkunga.
Mapema mwaka huu seŕikali ilifanya bila malipo ya uzazi wa mpango kwa wanawake wote wenye hadi miaka 26 – hatua ambayo iliwaathiri wanawake milioni tatu. Uzazi wa mpango hapo awali ulikuwa bure kwa wanawake na wasichana 18 au chini.
Macron aliongeza katika ukurasa wake wa Twitter kwamba tangazo la Alhamisi linakuja pamoja na hatua nyingine za afya.
Zinajumuisha uzazi wa mpango wa dharura bila malipo kwa wanawake wote katika maduka ya dawa, na uchunguzi wa bure wa magonjwa ya zinaa bila agizo la daktari, isipokuwa VVU, kwa wale walio chini ya umri wa miaka 26.