1.
Shirika la Under The Same Sun (UTSS) linalaani vikali kitendo
cha kinyama cha kukatwa kiganja cha mkono wa kuume cha mtoto mwenye albinism Baraka
Cosmas Rusambo (6); aidha, Prisca Shaaban, mama wa mtoto huyo kujeruhiwa vibaya
kwa mapanga kichwani kwenye shambulio la kikatili linalohusishwa na imani za kishirikina
lililotokea usiku wa Jumamosi Machi 7, 2015 kwenye Kijiji cha Kipeta, Kata ya Kiseta
wilaya ya Sumbawanga Vijijini mkoani Rukwa. Waathirika hao kwa sasa wanapata matibabu
kwenye Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya.
2. Wauaji hao wametokomea kusikojulika na kiganja cha mtoto huyo, huku Jeshi
la Polisi likishikilia watu saba wakituhumiwa kuhusika na shambulio hilo. Aidha
jeshi hilo limewahamishia mahali salama watoto wengine wawili wenye albinism wa
familia hiyo kwa ajili ya usalama wao.
3. Pamoja na hatua zilizochukuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali dhidi
ya matukio hayo ya kinyama kama vile Mh. Mizengo Pinda (Mb) – Waziri Mkuu ya kufungia
leseni za waganga wa jadi na hatimaye kuruhusiwa siku 30 kabla uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010; Mh. Mathias Chikawe (Mb)
– Waziri wa Mambo ya Ndani la kupiga marufuku
wapiga ramli chonganishi; na, hivi juzi Mh. Jakaya Kikwete – Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, aliyeapa kutokomeza unyama huo, bado matendo haya ya kinyama
yanaendelea kuiandama Tanzania, nchi inayotambulika kuwa kisiwa cha amani na kimbilio
la kila aliyevurugikiwa na amani nchini mwao.
4. Tunadhani ni wakati mzuri sasa wa kuja pamoja Serikali na wadau wote
ikijumuisha mashirika ya kutetea haki za binadamu ya nje na ndani ya nchi,
mashirika ya kidini, waandishi wa habari, mashirika ya watu wenye ulemavu,
wanasiasa, watu binafsi na wengineo ili kutafuta suluhu ya pamoja na ya kudumu kwa
maslahi na usalama wa nchi yetu Tanzania.
5. Ni wakati muafaka wa kufanyia kazi kauli na ahadi za Mh. Jakaya Kikwete
Rais wa Tanzania alizozitoa wakati akifanya mkutano na viongozi wa Chama cha
Albino Tanzania (TAS) Machi 5, 2015 Ikulu jijini Dar es Salaam kwamba serikali itafanya
kila iwezalo ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya pamoja ya wadau kutafuta njia muafaka
ya kukomesha mauaji haya yanayoiaibisha Jamhuri yetu ya Tanzania. Mkutano ulikubaliana
pia kufanyiwa mapitio kwa sheria zinazohusu uchawi na waganga wa jadi, vizuri utekelezaji
wa kazi hiyo ukaanza mara moja.
6. Tunapendekeza pia Waheshimiwa Wabunge wote wa maeneo yaliyoathirika na
kadhia hii walau kufanya kikao cha pamoja kujadili namna ya kutokomeza unyama
huo na hatimaye, kwa umoja wao, kuliomba Bunge la Jamhuri kujadili kadhia hii na
kuielekeza Serikali na vyombo vyake hatua na mbinu stahili
za kuchukua.
7. Aidha, kutekelezwa kwa sheria zilizopo bila shuruti ni jambo la
msingi sana. Kwa msingi huo, tunashauri waliokutwa na hatia na hatimaye kuhukumiwa
na mahakama zetu kwa mujibu wa sheria za Tanzania, basi adhabu zao zitekelezwe bila
kigugumizi chochote.
Imetolewa na Under The
Same Sun
Machi 11, 2015
Kwa
maelezo zaidi wasiliana na:
Vicky Ntetema, Mkurugenzi Mtendaji UTSS-TZ
Taasisi Road, Mikocheni B, Kwa Warioba
P.O. Box 32837, Dar es Salaam, Tanzania
Email: heviado35@gmail.com
T: +25522278024 Fax: +255222782356
Mob: +255753177752
/ +2557658600136