KITENDO cha aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto,
kutangaza bungeni kuwa anang’atuka ubunge, kilisababisha Bunge
kuzizima huku akipewa pole na wabunge wengi.
Hata hivyo mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Tundu Lissu na alikacha kumpa mkono.
Zitto ambaye alisoma barua aliyomwandikia Spika Anne Makinda, kuwa
analazimika kuachia wadhifa wa ubunge baada ya chama chake
kutangazia umma kuwa sio mwanachama wao, kulisababisha simanzi
kwa wabunge wengi ambao baada ya kikao cha Bunge kusitishwa wengi
walienda kumpa pole.
Hata hivyo, Zitto ambaye alikuwa amekaa pamoja na wabunge wengine
wa Chadema ambao wengi wao walimkumbatia kama ishara ya kumpa pole na kumtakia kila la heri aendako, Lissu na Msigwa
waligoma kumpa mkono mbunge huyo.
Kitendo cha Lissu na Msigwa kukacha kumpa mkono Zitto, kiliwafanya baadhi ya wabunge kupigwa na butwaa, lakini hata hivyo
Lissu alipoulizwa kwa nini hakumpa mkono mbunge mwenzake huyo, ambaye wametumika pamoja kwenye chama cha Chadema
kama viongozi, alisema yeye sio mnafiki.
Msimamo wa Zitto
Zitto aliliambia Bunge kuwa licha ya kutopokea barua rasmi ya kumjulisha juu ya uamuzi wa kumtimua uanachama, ameona ni
vyema akachukua uamuzi huo mapema kwa sababu jamii inaamini kwamba yeye sio mwanachama wa Chadema.
“Nashukuru, ushirikiano nilioupata kwa Bunge la Tisa na la 10, limenijenga na kunifanya niwatumikie Watanzania kwa kiwango
nilichostahili. “Naondoka katika Bunge hili lakini naamini nitarudi tena kwa mapenzi ya Mungu na tunaweza kuonana mwezi
Novemba,” alisema.
Kuhusu mafao mbalimbali anayostahili kupata kutokana na utumishi wake kwa Bunge, alisema hilo kwake si muhimu na
akaendelea kukumbusha kuwa kama Watanzania wanakumbuka ni siku nyingi yeye aliomba kuondolewa posho mbalimbali, ili
ziende kusaidia Watanzania wenye shida.
“Suala la mafao kwa sasa kwangu si kipaumbele, cha msingi niende msituni kufanya kazi ya siasa,” alisema Zitto ambaye
alipoulizwa na waandishi wa habari anaenda wapi, alisema kuwa siku sio nyingi kuanzia sasa atatangaza mustakabali wake wa
kisiasa.
Hata hivyo wachambuzi wa mambo ya siasa wanaamini kuwa mbunge huyo atajiunda na Chama cha ACT ambacho maswahiba
wake wengi ambao walitimuliwa Chadema, walienda kukianzisha.
Wanasiasa hao pamoja na Profesa Kitilya Mkumbo, Samson Mwigamba na wengineo wengi. Chama hicho licha ya uchanga wake
wa kisiasa, lakini kinaelezwa kuwa kina wafuasi wengi mkoani Kigoma hasa katika Jimbo la Kigoma Mjini ambako wachambuzi
wa mambo wanasema mwanasiasa huyo ana mpango wa kwenda kugombea katika jimbo hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na
Peter Serukamba (CCM)