WADAU wa elimu wameishauri serikali kupitia na kuangalia upya mchakato wa kubadili lugha ya kufundishia kuwa kiswahili kuanzia awali hadi vyuo vikuu.
Wadau hao wamedai kuwa kubadili lugha ya kufundishia kuwa kiwaswahili kutaleta madhara makubwa kwa elimu, kwani inaweza kuporomoka badala ya kuendelea kupanda.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Shule ya mchepuo wa kiingereza ya Maromboso, Olais Wavii Lukumay wakati akizungumza katika mahafali ya 16 ya darasa la saba shuleni hapo ambapo jumla ya wanafunzi 50 walihitimu.
Lukumay amesema serikali inapaswa kuwa makini sana katika mchakato huo kwani utachangia kuporomoka kwa elimu hapa nchini na kukosa wahitimu waliopikwa vizuri na hivyo kuchangia kukosa ajira na hatimaye nafasi nyingi kutawaliwa na wenzetu wa nchi jirani.
Amesema kutumia mchakato huo kwa sasa ni mapema kutokana na kuwa asilimia kubwa ya teknolojia tunakopa kwa wenzetu, hali ambayo inaonyesha wazi hatujakamilika ipasavyo katika sekta ya elimu bado juhudi zaidi zinahitajika kuboreshwa.
Lukumay amesema falsafa iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere isemayo ‘elimu imwandae mwanafunzi kupiga vita Maadui wa tatu ambao ni ujinga, maradhi, na umaskini,’ na mitaala iliyokuwa ikitumika wakati huo ilizalisha watu makini, wenye kujitambua na waliojaa haiba.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Bernad Kiduwa amesema kuwa, shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya wazazi kutokulipa ada kwa wakati, baadhi ya wazazi kutoshiriki kikamilifu kufuatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya ZZ Helping Hands Foundation, Don Schlesselman amewataka wanafunzi hao kutobweteka na elimu ya darasa la saba waliyoipata badala yake waongeze bidii ya kusoma zaidi hadi nyuo vikuu ili waweze kuwa na elimu nzuri na hatimaye kupambana na changamoto ya ajira hapa nchini.