MBUNGE wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ametangaza rasmi
kwamba hatagombea tena ubunge wa jimbo hilo wakati wa uchaguzi mkuu
mwaka huu.
Amesema ingawa alikuwa na nia ya kuendelea kuongoza jimbo hilo,
amelazimika kuacha kwa kuwa baadhi ya viongozi wa chama chake wilayani
Kasulu wanachafua jina lake bila sababu.
Machali alitangaza msimamo huo juzi mjini Kasulu alipohutubia mkutano wa hadhara.
“Kuna baadhi ya viongozi wachache wenye mawazo ya kijinga wanaotoka
Jimbo la Kasulu Vijijini wanashirikiana na Diwani wa Kata ya Kasulu
Mjini, Issack Rashid maarufu kama Mkemwema, kunitangaza kwamba
nimechukua uamuzi huu kwa sababu Mkemwema anataka kugombea ubunge katika
jimbo langu.
“Hiyo siyo kweli, ugomvi wangu mkubwa na hao watu umekuja kwa sababu
ninapiga vita ufisadi na mafisadi waliopo Wilaya ya Kasulu wanaojali
masilahi yao badala ya wananchi.
“Mimi sipendi usumbufu na wananchi ingawa wengine wanatembea huku na
huko wakisema ‘Machali hatujali’… hivi mnafikiri atatokea mbunge
atakayemaliza shida zenu zote?
“Kama atatokea huyo mbunge basi njooni mniombe silaha yangu mnipige
risasi nife kwa sababu naamini mbunge huyo hayupo na hatatokea katika
dunia hii.
“Watu wananipiga vita bila sababu kwa vile napingana nao, yaani wanataka
na mimi nipige madili kama wao, hiyo haiwezekani kwa sababu siko tayari
kuchafua jina langu.
“Wananisingizia mambo ya uongo, kama tatizo ni ubunge, basi nimeamua
sitagombea ili historia ije inihukumu kwa sababu ninapopinga ufisadi,
mafisadi na watu wa shetani wananipinga,” alisema Machali.
Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kutoa kauli hiyo, alikumbana na
upinzani mkali baada ya baadhi ya wananchi kupingana naye huku baadhi
wakilia.
Baadhi ya wananchi hao walisikika wakisema hawako tayari kukubaliana na mbunge huyo kwa kuwa wanaridhishwa utendaji kazi wake.
“Usiache kugombea maana wewe ndiyo kimbilio letu kwa sababu umetusaidia
katika maeneo ya Kagerankanda wakati tulipokuwa tukinyanyaswa na Mkuu wa
Wilaya mstaafu, Dan Makanga.
“Wewe ulisimama na sisi na leo Makanga hayupo tena, kwa hiyo, kama
usipogombea sisi wanyonge tutatetewa na nani,” walisikika baadhi ya
wananchi wakisema.
Baada ya wananchi hao kusema hayo, Machali alisimama tena na kuomba apewe muda atafakari maombi yao.
“Naomba nipewe muda wa kutafakari, wazee wangu nimewasikia, vijana
wenzangu nimewasikia na akina mama nimewasikia pia. Niacheni nitafakari
kwa sababu sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,” alisema Machali.
Katika mazungumzo yake, Machali alimshutumu pia Katibu Mkuu wa
NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe na Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni
Buyogela (NCCR-Mageuzi), kwamba wanachangia kukiharibu chama hicho
wilayani Kasulu.
“Viongozi wa Jimbo la Kasulu Vijijini hawawezi kunifanya mimi na wana
NCCR-Mageuzi Kasulu Mjini kuwa watumwa wa fikra zao mgando kwa sababu
nilikwenda darasani kusoma ili nielimike na elimu yangu niitumie kwa
manufaa na maendeleo ya jamii yangu.
“Ukweli unauma na wakati mwingine unatuponza wachache, kwa hiyo,
sitaogopa kusema ukweli na kutetea ninachokiamini hata kama nawaudhi
baadhi ya wenzagu,” alisema.
Pia aliwataka polisi wilayani Kasulu wasiwakamate ovyo waendesha bodaboda kwa kuwa bodaboda zimekuwa msaada mkubwa katika jamii.
Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi, Jimbo la Kasulu Mjini, Benedickt Rukubigwa,
alisema viongozi mzigo wa jamii ya Mkemwema, wanatakiwa kuvuliwa
madaraka kwa kuwa wanakiharibu chama chao.
“Mke Mwema ni bora akaombe uongozi CCM ambako kuna watu wa aina yake
kuliko kuendelea kukigawa na kukivuruga chama chetu,” alisema Rukubigwa.