Mwenyekiti wa taifa wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema),
Mh. Freeman Mbowe amezindua operesheni ya vijana wa chama hicho
inayojulikana kama ‘Shahada mkononi delete CCM’ ambayo itasimamiwa na
baraza la vijana wa chadema ( Bavicha ), huku akiwataka watanzania
kuacha kujengeana chuki za kisiasa na kuwa na upendo kama taifa moja
kwani vyama vya siasa ni mambo ya mpito.
Lengo la operesheni hiyo iliyozinduliwa wakati wa mkutano wa
hadhara uliofanyika katika viwanja vya mahakama ya mwanzo nguzo nane
mjini Shinyanga ni kuwahamasisha vijana wenye umri wa kupiga kura
kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa oktoba mwaka huu, kuwapa
fursa wananchi ya kuchagua viongozi bora watakaowaondoa kwenye lindi la
umaskini uliokithiri, kuleta haki na usawa kwa watu wote bila ubaguzi
pamoja na kujenga jamii iliyo huru kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali
zitokanazo na raslimali za taifa.
Mwenyekiti huyo wa Chadema ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya
upinzani bungeni na mbunge wa jimbo la hai mkoani Kilimanjaro, ametumia
mkutano huo wa hadhara kuwaasa askari polisi kuacha kutumiwa na chama
tawala kuwapiga mabomu na kuwamwagia maji ya kuwasha viongozi na
wanachama wa vyama vya upinzani wakati wanapokuwa katika harakati za
kutetea haki za wanyonge, yakiwemo maslahi ya askari polisi kwa madai
kuwa serikali ijayo itakuwa ni ya ukawa na wao ndio watakaoendelea
kuitumikia.
Uzinduzi wa operesheni hiyo umefanyika sambamba na ugawaji wa
baiskeli 17 zilizotolewa na mwenyekiti wa Bavicha taifa Patrobas Katambi
kwa uongozi wa kata zote za jimbo la Shinyanga mjini ambazo
zitarahisisha zoezi la uhamasishaji wa wananchi kwenda kwenye vituo vya
kujiandikisha.