Aliyekuwa
mwanasheria mkuu wa serikali Jaji Fredrick Werema amepokelewa
kijijini kwake baada ya kujiuzulu nafasi hiyo hivi karibuni.
Jaji
Werema amepokelewa kijijini kwake baada ya kujiuzulu nafasi hiyo
hivi karibuni huku wananchi wa kijiji hicho wakiwataka
watuhumiwa wote katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow
kujiuzulu nafasi zao ili kulinusuru taifa kuingia katika mgawanyiko
na machafuko ambayo wamedai yanaweza kuhatarisha amani.
Wakizungumza
baada ya kumpokea Jaji Werema muda mfupi baada ya kuwasili
katika kijiji hicho cha Kongoto tarafa ya Kiagata mkoani Mara,
wananchi hao wamempongeza kiongozi huyo kwa kuchukua hatua ya
kujiuzulu nafasi hiyo ya uanasheria mkuu wa serikali.
Wananchi
hao pia wamesema ni jambo la busara kwa kiongozi wa umma
kuchukua uamuzi kama huo katika kulinusuru taifa lake hasa
baada ya kutuhumiwa katika sakata hilo.
Kwa
upande wake Jaji Fredirick werema, akizungumza na wananchi hao
amesema hawezi kuteteleka kwa uamuzi wake wa kujiuzulu huku
akisema ni jambo la busara kama kiongozi wa umma unapohusishwa
na tuhuma zozote kukubali kwa hiari yako kuwajibika ili
kulinda maslahi ya taifa.
Kuhusu
chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kushinda katika kijiji
chake kwa nafasi ya uenyekiti wakihusisha ni kutokana na sakata
la Escrow, Jaji Werema amesema hatua hiyo imetokana na wananchi
kuchoshwa na baadhi ya viongozi wa CCM katika eneo hilo hivyo
kuomba wananchi kumpa kiongozi huyo ushirikiano katika kutimiza
wajibu wake.
