Rais Uhuru Kenyatta amemwachisha
kazi waziri wa usalama Joseph Ole Lenku na kumpendekeza waziri mpya wa
usalama Joseph Nkaiseri kuchukua nafasi hio.
Wakati huohuo mkuu wa
polisi nchini Kenya inspekta generali David Kimaiyo amejiuzulu kutokana
na shinikizo dhidi yake afanye hivyo kwa kushindwa kukabiliana na utovu
wa usalama nchini.
Rais Kenyatta alisema kuwa baada ya mazungumzo
na Bwana Kimaiyo alikubali 'kustaafu' mapema kutoka kwa majukumu yake
kwa sababu za kibinafsi.
Rais alitoa tangazo hilo wakati
akihutubia taifa kufuatia shambulizi la hapo jana dhidi ya wachimba
migodi 36 waliouawa na Al Shabaab mjini Mandera Kaskazini ya Kenya.
Rais pia alitangaza kuwa amekubali ombi la Generali wa polisi David Kimaiyo kuachia wadhifa wake.
Kimaiyo na Ole Lenku wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo za kuachia ngazi kufuatia kukithiri kwa utovu wa usalama nchini.
Hatua
ya kuwatimua kutoka katika nyadhifa zao wawili hao bila shaka litakuwa
jambo la kuridhisha kwa wakenya wengi ambao wamekuwa wakilalamikia utovu
wa usalama na kuwataka waondoshwe ofisini.
Uteuzi wa Joseph
Nkaisery kama waziri mpya wa usalama ni jambo jipya kwani atakuwa
mwanasiasa wa kwanza kutoka kwa upinzani kuwa ndani ya serikali.
Alipokuwa
anahutubia nchi,Rais Kenyatta aliwasihi wabunge kuongeza mda wa vikao
vyao vya leo ili kumhoji na kumkagua Nkaisery aliyeteuliwa kuchukua
nafasi ya waziri mpya wa usalama na maswala ya ndani ili wamuidhinishe.