Mapigano makali yamezuka kati ya jamii mbili za wafugaji katika Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na kusababisha vifo vya watu zaidi ya tisa.
Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Kihale,
Tarafa ya Chole wilayani Kisarawe na yamehusisha jamii mbili za wafugaji
wa kabila la Wasukuma na Wabarbaig ‘Mang’ati’.
Hata
hivyo, imeelezwa kuwa ni miili ya wafugaji watano tu ndiyo iliyopatikana
huku maiti wanne hawajulikani walikotupwa na watuhumiwa.
Kamanda
wa polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema vuguvugu la vurugu hizo
lilianza Novemba 26, baada ya mfugaji wa Kimang’ati kudaiwa kuiba
ng’ombe zaidi ya watano toka kwenye zizi la mfugaji Wakisukuma
Kamanda
Matei alisema mapigano hayo yalizuka baada ya wafugaji wa Kisukuma
kuamua kufanya msako wa ng’ombe hao waliodaiwa kuibiwa na kupelekwa
katika kijiji cha Kihale.
Alisema baada ya wafugaji hao
ambao wengi wao ni vijana walipombaini mwizi wao waliamua kumpa kipigo
kikali kilichomsababishia kifo.
Mauaji hayo yaliamsha hasira ya Wamang’ati walioamua kulipiza kisasi na kusababisha vifo vya watu wengine wanane.
Kamanda Matei alisema maiti zilizopatikana, ziliokotwa shambani na zingine zilitupwa msituni.
“Maiti wanne hawajapatikana bado na polisi kwa kushirikiana na wakazi wa kijiji hicho wanaendelea kuzitafuta,” alisema Matei.
Alisema
uchunguzi bado unaendelea ili kubaini chanzo na watu waliohusika katika
mauaji hayo. “Hata ndugu wa hawa marehemu wanaogopa kujitokeza
kuwatambua ndugu zao kwa kuhofia kushambuliwa au kuhusishwa na mauaji
hayo, kwa hiyo hata majina ya marehemu hatujayapata bado,” alisema
Matei.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye
pia ni mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza ameelezea kusikitishwa na
kitendo hicho na kuagiza polisi kuhakikisha wanafanya msako mkali ili
kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika vurugu hizo.
Adam
Ng’imba ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, amesema
tayari kikao cha usuluhishi kilichowakutanisha wafugaji wa pande zote
mbili kilifanyika jana na jitihada zingine za kutafuta suluhisho la
mapigano zinaendelea kufanyika, ikiwa ni pamoja na kutafuta njia ya
kuwabaini wote waliohusika.