Aziza
Hassani akimuuguza mtoto wake Zuhura Rajabu (17) aliyelazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Handeni, baada ya kuungua mwili mzima walipokuwa
wakifanyiwa dawa kwa mganga wa kienyeji na mama huyo alipata majeraha
madogo kichwani.
“Ama
kweli hujafa hujaumbika,” walisema walimwengu wakiwa na maana kubwa
kwamba tangu kuzaliwa hadi kufa hupitia au kukumbwa na mabadiliko
mbalimbali, lakini litakavyotokea au lini ni siri ya Mungu pekee.
Binadamu
anaweza kuzaliwa bila kasoro yoyote na kujijengea matumaini ya kutimiza
malengo yake bila wasi wasi, lakini akapatwa na mkasa utakaofuta ndoto
zake zote.
Hivi
ndivyo ilivyotokea kwa msichana Zuhura Rajab mwenye umri wa miaka 17,
ambaye kwa mfumo wa maisha ya Kitanzania hajatimiza ndoto yake hata
moja, awe akiishi kijiji au mjini kwani hajafikisha umri wa kujitegemea.
Mbali
na ukweli huo, maisha na ndoto za Zuhura zimefifia ghafla baada ya
kuingizwa na babu yake kwenye imani iliyogharimu maisha yake na sasa
anauguza majeraha kutokana na kuungua moto huku wataalamu wakisema
asilimia 72 ya mwili wake umeathirika kwa moto.
Mkasa
uliomkuta Zuhura hataweza kuusahau maishani mwake kwani maelezo ya
kitaalamu yanaonyesha kuwa akipona, asilimia chache ya viungo vyake
vitaweza kufanya kazi kwa usahihi kwani majeraha ya moto husababisha
ngozi kujikunja.
“Mimi
na wanangu tuliitwa nyumbani, tulifika kwa mganga mimi, mama yangu
mzazi pamoja na watoto wangu wawili. Sisi ndiyo tuliingizwa kwenye
shimo, ila baba hakuingia bali alibaki juu na yule mganga. Hadi tukio
linatokea, hakusogea kabisa kwenye lile shimo.”
Ndivyo
anavyoanza kusimulia Aziza Hassani (35) mama wa watoto wawili ambaye
yeye na mtoto wake mmoja wamepona kwenye tukio hilo la moto uliowashwa
kwa makusudi na mganga wa kienyeji nao kuambiwa watoke huku moto ukiwaka
na atakayeshindwa, atakuwa amekamatwa na dawa ya mganga huyo.
Anasimulia
kwamba November 26 alipigiwa simu na mama yake mzazi aliyemweleza kuwa
kuna dawa (tambiko) la wanafamilia hivyo yeye na wanawe kutakiwa kwenda
nyumbani kwa ajili ya shughuli hiyo.
Anaeleza
kuwa alifika nyumbani mapema siku hiyo hiyo akiitika wito wa wazazi
wake na kuelezwa kwamba anapaswa kushiriki kwenye dawa kesho yake
Novemba 27, agizo ambalo alikubaliana nalo, lakini alipouliza ni dawa ya
nini alielezwa kuwa ni tambiko.
Aziza
anaeleza kuwa walifika kwa mganga huyo na kuanza kufanyiwa dawa
iliyofanyika ndani ya shimo ambalo liliezekwa kwa nyasi kavu juu yake na
kuachwa nafasi ndogo mfano wa mlango, ambao ndiyo walioutumia kuingilia
ndani yake na dawa ilifanyika.
“Mganga
alianza kufanya kazi yake sisi tukiwa ndani ya shimo. Tulikuwa mimi
mtoto wangu mdogo Hassan Rajab (4), Zuhura Rajabu (17) pamoja na mama
yangu mzazi, Hadija Abdallah(65) ambaye ndiye aliyeniita katika dawa
hiyo,” anasema Aziza.
Anafafanua
kuwa iliwachukua zaidi ya nusu saa wakiwa ndani ya shimo hilo hadi
hatua ya mwisho ya dawa hiyo na walimwona mganga huyo akiwa amemaliza
kufanya mambo yake na kubaki pembeni ya shimo walilokuwamo.
Baada
ya muda walidhani mganga ameshamaliza na kumuuliza wanaweza kutoka,
lakini aliwajibu dawa bado inaendelea na ghafla mganga huyo aliwasha
moto juu ya zile nyasi.
“Moto
mkubwa ukaanza kuwaka ndipo mganga akatuamrisha tutoke shimoni huku
moto ukiendelea kuenea hadi mlangoni,” Aziza anasimulia kwa uchungu.
Anasema
kuwa baada ya kauli hiyo ya mganga kuwa waanze kujiokoa, alianza
kumrusha nje mtoto wake mdogo (Hassan) kisha kuanza harakati za
kumsaidia mama yake na mtoto wake mkubwa (Zuhura) lakini hakufanikiwa
kutokana na moto kuwa mkubwa.
“Hivyo mimi niliungua kichwani, mama yangu na mwanangu Zuhura miili yao ikaungua vibaya,” anasimulia.
Anaeleza
kuwa baada ya moto kupungua, yule mganga na baba yake walikuja
kuwasaidia kuwatoa ndani ya shimo huku wenzake wakiwa wameshaungua kiasi
cha kushindwa kufanya lolote.
Baada
ya kutolewa majeruhi hao baba yake na mganga walimshauri wasipeleke
majeruhi hospitali wakawaeleza kuwa kuna daktari wao atakwenda kuwatibu
katika kijiji cha jirani na hapo walimhakikishia kuwa majeruhi hao
watapona.
Hata
hivyo, Aziza anasema kuwa kwa daktari huyo hakuna kilichofanyika kwa
zaidi ya siku tatu na ilipofika Desemba mosi mama yake alifariki dunia
hapo hapo kijijini huku hali ya mtoto wake ikizidi kuwa mbaya kutokana
na kukosa tiba.
“Kwa
huyo mganga hakuna tiba waliyopata zaidi ya kubandikwa pamba kwenye
vidonda vyao kwa siku zote tatu. Mama alifariki dunia kutokana na
majeraha yake kuendelea kila siku na maumivu makali,” anasema Aziza.
Anasema
kwamba jambo baya lililokuwa likiendelea kwa daktari huyo ni vidonda
vya majeruhi kuanza kuharibika na kutoa wadudu hali anayosema ilianza
kumtisha zaidi na kuanza kukata tamaa ya kupona.
Hospitali
Akizungumza
kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Handeni, Muuguzi
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni Mwanaidi Semboja anasema kuwa
walimpokea mgonjwa huyo (Zuhura) akiwa katika hali mbaya huku vidonda
vyake vikiwa havijapata tiba yoyote.
Anasema
baada ya kumpokea walianza kumpa tiba za kitaalamu zaidi ikiwemo
kumpunguzia maumivu yaliyotokana na kuungua sehemu kubwa ya mwili wake
hivyo kushindwa kufanya lolote.
“Kwanza
tulianza kumpatia dawa za kumpunguzia maumivu kwani aliletwa akiwa
kwenye hali mbaya sana kutokana na kutofungwa vidonda. Kitaalamu ili
kuzuia baridi, tulianza kufanya hivyo na baada ya siku kadhaa mgonjwa
aliendelea vizuri,” anasema.
Muuguzi
huyo anasema kuwa kitaalamu binti huyo ameungua asilimia 72 na kwamba
mgonjwa kama huyo anatakiwa kuwa na uangalizi maalumu kwa muda wote.
Semboja
anasema kuwa wanawashukuru wasamaria wema waliotoa taarifa polisi ambao
walifika walipohifadhiwa majeruhi hao, kisha kuwachukua kuwapeleka
hospitali, ambapo yeye Aziza anaendelea vizuri, huku Zuhura akiendelea
kupata tiba na kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa, Bombo mjini Tanga.
Wananchi
Aziza
Mkomwa mkazi wa wilayani Handeni anashauri akisema kuwa ni vyema
wananchi wakamrudia Mungu kwa kumwamini na kufanya ibada misikitini au
kanisani, badala ya kuendeleza imani potofu ikiwamo matambiko.
Anasema
ni muhimu kila mtu asimamie kwenye imani yake ya kidini kwa kufuata
yale ambayo vitabu vitakatifu vinamwongoza badala ya kwenda kinyume na
maagizo ya Mungu hata kukutwa na matukio ya ajabu kama yaliyomkuta Aziza
na familia yake.
Polisi
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraisser Kashai anathibitisha kutokea kwa
tukio hilo akisema kuwa mtuhumiwa amekamatwa na hatua zaidi kuchukuliwa.
Chanzo:Mwananchi