Serikali imetakiwa kuwa makini na
kuchukua tahadhari za kutosha kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa
kuweka vifaa vya kupima na kubaini watu wenye ugonjwa huo hapa nchini
kuliko hali ilivyo kwa sasa kupeleka sampuli za watu wanaohisiwa kuwa na
ugonjwa huo nchini kenya.
Balozi wa majanga Afrika na mwenyekiti cha chama cha NCCR Mageuzi
Mh.James Mbatia ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo
la vunjo na kusema kuwa bado serikali haijachukua hatua za kutosha za
kukabiliana na ugonjwa huo na kwamba athari zake kidunia ni kubwa
hususani katika sekta ya utalii ambayo inategemea wageni kutoka nje ya
nchi.
Amesema ni vema serikali ikaacha kuingiza masuala ya kisiasa katika
ugonjwa wa Ebola na kwamba endapo watalii watasikia Tanzania haina
maabara ya kupima sampuli za ugonjwa huo athari zake kiuchumi ni kubwa
hapa nchini hususani mkoa wa Kilimanjaro ambao unategemea utalii.
Kutokana na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuendelea kupata hofu
ya ugonjwa huo kufuatia taarifa za uwepo wa mgonjwa anayehisiwa kuwa na
dalili za ugonjwa wa Ebola katika manispaa ya Moshi wameiomba serikali
kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo.