Mjumbe
wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni mwanachama wa CHADEMA, Leticia
Nyerere (kushoto) akitoka kujaza fomu ya mahudhurio ya vikao vya Bunge
hilo huku akisindikizwa na mjumbe mwenzake, Steven Ngonyani
**************
**************
Katika
mijadala mbalimbali, msemaji wa Ukawa ambaye pia ni Mwanasheria wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekuwa
akisisitiza kwamba wajumbe wa Ukawa na hasa kutoka Chadema,
hawatahudhuria Bunge Maalumu la Katiba.
Aidha,
wiki iliyopita Chama cha Wananchi (CUF) kilisambaza waraka kwa vyombo
vya habari, kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika
chama hicho, kutohudhuria vikao vya Bunge hilo, vilivyoanza juzi.
Hata
hivyo, katika kile kilichoonesha kutoungwa mkono kwa viongozi wa Ukawa
ndani ya vyama vyao, baadhi ya wabunge waliozuiwa kushiriki vikao hivyo,
wameonekana bungeni wakijisajili, kuashiria ushiriki wao bila kujali
viapo na makatazo ya viongozi wao.
Leticia, Shibuda
Jana
saa 5:55 asubuhi mjumbe wa bunge hilo, Leticia Nyerere ambaye ni Mbunge
wa Viti Maalumu kutoka Chadema, aliwasili kwenye viwanja vya bunge na
kwenda moja kwa moja kwenye eneo la kujisajili na kukamilisha taratibu
zinazotakiwa.
Hata hivyo, Leticia hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari, wakati akienda kujiandikisha.
Hata wakati anatoka kukamilisha taratibu zinazotakiwa za kujisajili, pia alikataa kupigwa picha. “Unajua kwamba kunipiga picha bila idhini yangu ni ‘illegal (kinyume na sheria)? Sitaki,”
alisema huku akielekea mlango wa kutokea, ambako alikutana na mjumbe
mwingine wa bunge hilo, ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven
Ngonyani (CCM), aliyekuwa akitoka pia kujisajili.
Ngonyani
alisalimiana na Leticia na wakawa wanaongozana kutoka eneo la Bunge.
Ngonyani alionekana mwenye furaha baada ya mjumbe mwenzake, kukamilisha
taratibu za usajili.
Mapema
juzi, wajumbe wengine wa Bunge hilo, Mbunge wa Maswa Mashariki, John
Shibuda (Chadema) na Clara Mwatuka ambaye ni Mjumbe wa Viti Maalum
kutoka CUF, nao walijisajili kushiriki vikao hivyo.
Wanaojishauri
Jana
asubuhi pia zilikuwepo taarifa bungeni kwamba Mbunge wa Mpanda Kati,
Said Arfi (Chadema), naye alijisajili. Lakini, akizungumza na mwandishi
kwa simu, alisema alifika Dodoma, lakini hajaamua kama ajisajili ili
ashiriki vikao au la.
“Sijajisajili
bado, sio kweli, sijaamua nichukue huo uamuzi wa kushiriki au la, kama
nikitaka kujisajili nitasema, ila kweli nipo Dodoma,” alisema Arfi ambaye alijiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema hivi karibuni.
Zitto
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), hivi karibuni aliibuka na kupingana na harakati za Ukawa.
Zitto
alikaririwa akisema, hana uhakika wala hauamini Ukawa kama utakuwa
umoja endelevu hadi kufikia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara
ya kwanza vyama vya upinzani, kuungana na kugawanyika.
Zitto
alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast,
kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds cha jijini Dar es Salaam,
ambapo alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi na si Katiba
pekee.
Alisema
siku zote Watanzania, wamekuwa wakipenda kuwa na upinzani imara, ambao
watu wanaweka tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya chama ambacho
kinaongoza, lakini haoni kama Ukawa utaendelea hadi kufikia kipindi cha
Uchaguzi Mkuu.
Alisema
hatua ya kusimama kwenye ajenda moja ya Katiba, haitausaidia umoja huo,
kwani kipindi cha Uchaguzi Mkuu, kinakuwa na ajenda nyingi.
Alisema wananchi watapenda kusikia masuala ya kushughulikia rushwa, matumizi ya rasilimali, maji, umeme, afya na barabara.
“Mambo haya ndiyo yatakayowafanya wananchi waamue namna gani watakabidhi dhamana ya uongozi, si suala la Katiba pekee,” alisema Zitto.
Samuel Sitta
Juzi
wakati akizungumza bungeni, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alisema
zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa bunge hilo, walikuwa wamejiandikisha,
ingawa hakutaja namba kamili. Pia, majina ya waliojiandikisha,
hayatolewi kwa vyombo vya habari.
Kwa
mujibu wa Sitta, wajumbe wakishajisajli, fedha zao zinawekwa kwenye
akaunti zao moja kwa moja kwa wale wenye akaunti ya Benki ya NMB. Wale
ambao hawana akaunti NMB, wanachukua mkononi.
Aidha, katika mitandao mbalimbali, kulikuwa na taarifa kuwa karibu wajumbe 50 kutoka Ukawa, walikuwa wameshafika Dodoma, ingawa hawakuonekana katika viwanja vya Bunge.
Taarifa
zingine zilieleza kuwa katika vyama hivyo, baadhi ya wabunge
wanalalamikia viongozi wao, kususia Bunge Maalumu kutokana na ajenda zao
binafsi, huku wao wakitakiwa na wapiga kura wao kuhudhuria bunge hilo.
Wajumbe
waliojiundia kundi la Ukawa ambao wanatoka vyama vya NCCR Mageuzi,
Chadema na CUF walisusia vikao vya bunge hilo Aprili mwaka huu, kwa kile
walichodai halijadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba.
Bulembo
Wakati
huohuo, Mjumbe wa Bunge hilo, Alhaji Abdallah Bulembo, alisema anaamini
Katiba itapatikana na Ukawa watazidi kupasuka kadri muda unavyoenda.
“Tayari
wameanza kujiandikisha, nasema watagawanyika siku si nyingi na Katiba
itapatikana, hotuba ya Mwenyekiti (Sitta) juzi ilikuwa nzuri sana na
imetoa mwelekeo wa mzuri,” alisema Bulembo, ambaye anatoka Kundi la Wajumbe 201, walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Leo
(jana) tumeanza kujadili rasimu kwenye kamati, tunajadili bila jazba,
tunaenda vizuri na naamini mambo yatakamilika kama tunvyopanga." Mwandishi alimtafuta Msemaji wa CUF, lakini mara zote simu yake haikupatikana.
Baadaye,
mwandishi alimpigia simu Jusa Ismail na kumuuliza juu ya tukio la
Mbunge wa CUF, Clara Mwatuka kujisajili katika Bunge Maalum la Katiba,
linaloendelea na vikao vyake huko Dodoma.
Jusa alijibu, “Siwezi
kukisemea Chama. Mimi ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama, naomba
umtafute Naibu Katibu Mkuu wa chama, Magdalena Sakaya, atakupa
ufafanuzi”.
Ndipo,
mwandishi alimpigia simu Sakaya, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa
CUF. Lakini, mara zote simu yake ilikuwa haipatikani.
Kwa
upande wa Chadema, mwandishi alimpigia simu Mkurugenzi wa Uenezi wa
Chadema, John Mnyika ili atoe ufafanuzi wa juu wa wabunge wao wawili,
Leticia Nyerere na John Shibuda, kujisajili kwenye Bunge Maalum la
Katiba mjini Dodoma.
Hata hivyo, simu zote mbili za Mnyika, hazikupatikana.