JESHI la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na askari wa kitengo cha uhalifu wa kimtandao wamemkamata mfanyabiashara Merry Duwe (40), mkazi wa Mwengemshindo, Manispaa ya Songea akiwa na watoto wawili wanaodaiwa kuibwa Oktoba 4, mwaka huu, Salasala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Chilya, alisema walimkamata Oktoba 8 eneo la Kijiji cha Litola wilayani Namtumbo ambako alikuwa na watoto hao wenye jinsi ya kike na kiume.
Alifafanua kuwa Oktoba 4, mwaka huu, eneo la Salasala jijijni Dar es Salaam, mtuhumiwa alikwenda nyumbani kwa Zenatha Majaliwa, mama wa watoto walioibwa na kumkuta mume wake ambaye alimwomba hifadhi ya kulala na kumruhusu.
Alisema siku iliyofuata, asubuhi baba wa watoto hao alikwenda kazini na kuwaacha na binti wa kazi, kitendo kilichompa nafasi mtuhumiwa kuwachukua watoto hao kwa kuwadanganya kuwa anakwenda kuwanunulia pipi na kutokomea nao kwa usafiri wa bajaji.
Alisema baadaye alishuka kituo kilichofuata na kupanda daladala hadi Ubungo ambako inadaiwa alipata usafiri wa lori uliowafikisha Morogoro.
Kamanda Chilya alisema mtuhumiwa baadaye alipata usafiri mwingine wa basi kutoka Morogoro hadi Iringa na kupanda gari lingine la abiria ambalo liliwafikisha Njombe Mjini na kupata usafiri mwingine hadi Songea.
Alifafanua kuwa baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa ya kuibwa kwa watoto hao, lilianza juhudi za kuwatafuta.
Alisema kuwa baadaye jitihada zilifanyika kwa ushirikiano kati ya askari polisi wa kitengo cha uhalifu wa kimtandao, Polisi Ruvuma pamoja wazazi wa watoto na kufanikisha kumkamata mtuhumiwa akiwa na watoto hao ambao walikutwa wakiwa katika hali nzuri, japo wanaendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi wa afya zao.
Mama mzazi wa watoto hao, akizungumza na Nipashe jana, alisema mtuhumiwa kabla ya kuwaiba wanawe, alikuwa na uhusiano naye katika shughuli za biashara.
Alisema kuwa Oktoba 4, mwaka huu, asubuhi mtuhumiwa Merry aliwaiba watoto na kutokomea nao kusikojulikana na baadaye alipigiwa simu kuwa watoto wote wawili anao na hawezi kuwarudisha mpaka alipwe fedha zake, jambo ambalo lilimlazimu aendelee kumtafuta licha ya kuwa tayari alikuwa ameshatoa taarifa polisi kuhusu kuibwa kwa watoto wake.
Zenatha alilishukuru Jeshi la Polisi kwa jitihada walizozifanya za kufanikisha kuwapata watoto wake wakiwa salama kwa kuwa alishakata tamaa kuwapata.
Chanzo: Nipashe Digital