Suala la Mahakama ya Kadhi limeleta mjadala mkali katika majadiliano na wabunge wameamua suala hilo lisiingizwe kwenye Katiba.
Mjadala
huo mkali uliibuka katika Kamati namba Saba ilipojadili sura ya Nne ya
kwenye rasimu hiyo inayozungumzia juu ya uhuru wa imani ya dini ambapo
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hassan Ngwilizi alisema baada ya mjadala
mkali wamekubaliana kutoingizwa kwenye Katiba.
“Changamoto
kubwa iliyojitokeza ni wakati tukijadili suala la Mahakama ya Kadhi
kuna baadhi ya wajumbe walitaka liingizwe kwenye Katiba na wakanukuu
Katiba ya Zanzibar imeruhusu Mahakama hiyo lakini tukaona si kweli na
baada ya mjadala mkali tumekubaliana Mahakama ya Kadhi iwe nje ya
Katiba,” alisema.
Ngwilizi
alisema jana kuwa Kamati yake imeshakamilisha upigaji kura na akidi
kutimia kwa kila sura kwa kupata theluthi mbili kwa upande wa Zanzibar
na Bara, wameondoa kipengele cha uraia pacha kwenye rasimu ya Katiba na
kupendekeza kutungwe sheria itakayoingiza uraia huo kwa kuzingatia mambo
muhimu ya utoaji wa uraia huo.
Alitaja
maoni mapya yaliyozingatiwa kwenye Kamati yake kuwa ni pamoja na ardhi
kuundiwa sura yake na masuala ya serikali za mitaa lakini akaongeza “suala la kuwepo machifu au chochote kuhusiana na machifu hatukujadili”.
Juzi
Umoja wa Machifu Tanzania uliwasilisha mapendekezo yao wanayotaka
yaingizwe kwenye rasimu ya Katiba ikiwemo watambuliwe na washirikishwe
kuanzia Serikali za Mitaa kwenye kupanga mikakati ya kijamii, kuundwe
Tume ya Utamaduni na lugha za asili zilindwe na kuendelezwa.
Kuhusu vipengele vilivyobadilishwa alisema “tumeondoa
serikali tatu na kuweka muundo wa serikali mbili na chemba za Bunge
tumetaka mbili kama ilivyo sasa yaani Baraza la wawakilishi na Bunge la
Jamhuri ya Muungano”.
Naye
Mjumbe Abdallah Bulembo kutoka kamati hiyo namba Saba alisema kwenye
muundo wa Bunge kulitokea ubishi mkali kwani wapo waliotaka wabunge
watano kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wakawakilishe Bunge hili
kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar lakini baada ya mjadala mkali
wakakubaliana muundo wa mabunge mawili ubaki kama ilivyo sasa.
Alisema kulikuwa na mvutano mkali kwenye suala la ardhi na kusisitiza “wengi
waliipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kuweka sheria kwamba
kwenye kiwanja chako kukionekana madini unaweza kuuza asilimia 80 na
asilimia 20 inabaki kwa mwenye kiwanja hivyo anakuwa mmoja wa
wabia…mtaona bungeni suala la ardhi litakuwa na mjadala mkali na
itachukua muda mrefu”.
Mjumbe
Kaika ole Telele alisema suala la mgombea binafsi lilileta mvutano
mkali na mwishowe wakakubaliana awepo kwani halina madhara na kuzuia ni
kuminya demokrasia kwani hata Marekani wameruhusu na hajawahi kushinda.
Alisema wamekataa mabunge matatu na kukubaliana mabunge mawili kama ilivyo sasa na serikali mbili na kufafanua “suala
hili tulijadili kwa siku mbili na hawa wajumbe kutoka Zanzibar
waliridhika tubaki na mabunge mawili baada ya kuvutana
sana…tumekubaliana pia Rais apunguziwe madaraka ya uteuzi, asiteue wakuu
wa mashirika na taasisi aishie kumteua Mwenyekiti wa Bodi tu”.
Kuhusu
wafugaji alisema wamekubaliana kuwe na ardhi ya wafugaji ili waache
kutangatanga na hata maeneo ya mapori ambayo hayana hata digidigi
yarudishwe kwa Rais na wapewe wafugaji ili watulie.
Kwa
upande wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge, Samia Suluhu Hassan alisema
Kamati ndogo ya Uongozi imeshafanyia kazi juu ya Mahakama ya Kadhi,
Uraia pacha na muundo wa Bunge baada ya kukutana na wataalamu katika
maeneo hayo na leo wanakutana na makatibu wakuu wa wizara za fedha kwa
Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kujadiliana juu ya kamati ya pamoja ya
fedha ya muungano.