Mrithi wa Rais Jakaya Kikwete, atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani, ameanza kuandaliwa makao yake Ikulu, yatakayomwezesha si tu kuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania tajiri, bali pia kuanza kazi bila viporo vya miradi ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Tayari,
Rais Kikwete ameshatangaza azma yake ya kutaka kuwa Rais wa mwisho wa
Tanzania masikini na katika tangazo hilo alilolitoa hivi karibuni
Marekani, alisema muda wake uliobakia Ikulu, kazi kubwa ni kuandaa
misingi ili Rais ajaye, awe Rais wa Kwanza wa Tanzania tajiri.
Juzi
katika kujenga misingi hiyo, Rais Kikwete alipokuwa akiweka jiwe la
msingi katika ujenzi wa barabara ya lami kati ya Magole hadi Turiani,
mkoani Morogoro, alisema atahakikisha kila mradi wa maendeleo
ulioanzishwa wakati wa uongozi wake, unamalizwa.
Barabara hiyo ya Magole mpaka Turiani, ina urefu wa kilomita 48.6 na itagharimu Sh bilioni 49.44.
“Tulipoahidi
kuwa tutajenga barabara za lami ili kuunganisha mikoa na wilaya, watu
wasiotutakia mema walitubeza...lakini sasa wenyewe wanaona nini
tumekifanya,“ alisema Rais Kikwete mbele ya wananchi waliofurika eneo la Mvomero.
Rais
alisema, barabara nyingi za lami zimejengwa baada ya kupata Uhuru mwaka
1961 na nyingi katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Nne ulioanza
2005.
“Wakoloni
walituachia barabara chache za lami, kuja Morogoro kutoka Dar es Salaam
na Dar es Salaam kwenda Tanga pamoja na za mijini katika maeneo
waliyokuwa wakikaa wazungu ...hizo zingine zote mnazoziona zimejengwa
baada ya Uhuru,” alisema Rais kwa wananchi hao.
Aliendelea
kusisitiza na kurudia kauli yake, kwamba atasimamia miradi ya barabara,
umeme, maji ma mingine, ili imalizwe kabla ya kustaafu Urais na kama
kutatokea ikabaki kwa bahati mbaya, basi iwe michache isiyokuwa mzigo
kwa mrithi wake.
Rais
alisema ziara yake ya Mkoa wa Morogoro ilipokuwa ikianza Agosti 20
mwaka huu, aliagiza apangiwe kwenda maeneo ambayo hayajafikiwa na
viongozi wa kitaifa wa ngazi ya Rais.
Baada
ya kufika katika maeneo hayo, ikiwemo Nyandira na Kibati katika Wilaya
ya Mvomero, Kisanga na Msolwa katika Wilaya ya Kilosa na Kisaki na
Kinole, katika Wilaya ya Morogoro, amejionea mwenyewe kasi ya maendeleo
inayohitajika kupelekwa vijijini.
“Bado
nina muda, katika bajeti ijayo tunaongeza fedha katika miradi ya
maendeleo, ili kuwezesha ifikie mwisho na kama itakuwa bado, basi iwe ni
michache kuepusha mzigo kwa mrithi anayefuata,“ alisisitiza Rais Kikwete.
Hivi
karibuni Rais Kikwete alipokuwa akizungumza katika Kituo cha Kimataifa
cha Maendeleo mjini Washington DC, Marekani, alisema anataka na
anatamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania, kuongoza nchi ambayo ni
masikini.
Ili
kutimiza lengo lake hilo, Rais Kikwete alisema atatumia muda wake
uliobakia katika uongozi, kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo, ambao ni
kuhakikisha Watanzania wananufaika na gesi asilia.
“Rasilimali
ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na
umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu
kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na
mwisho
wa kipindi changu cha uongozi, ni kuiongoza nchi yetu kuelekea kwenye
njia hiyo, ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi
kwa wananchi wetu,” alisema.
Akimzungumzia
Rais ajaye, Rais Kikwete akiwa Marekani, alisema ili Watanzania
wanufaike na mapato ya gesi, ni muhimu kuwepo na uongozi imara, ambao
utakuwa tayari kuchukua uamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyosonga mbele.
Alisema
anataka kufanya kila linalowezekana katika kipindi chake kilichobakia
cha uongozi, kuhakikisha anaanzisha na kuanza kujenga taasisi na kuweka
kanuni sahihi za kusimamia rasilimali ya gesi asilia.
Tayari
Serikali imeweka hadharani mapendekezo ya Sheria ya Mgongano wa
Maslahi, ambayo itawalazimisha viongozi na watumishi wa umma,
kutenganisha uongozi pamoja na utumishi wao kwa umma na biashara, ili
kuzuia ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma unaoendelea kutokea
nchini.
Katika
mapendekezo hayo yaliyoanza kujadiliwa na wadau mbalimbali, wakiwemo
viongozi wa sasa, viongozi wote na watumishi wa umma, watatakiwa
kuchagua kati ya mali na biashara zao na nafasi ya utumishi wa umma.
Uchaguzi
huo utafanyika kwa namna mbili; moja kukabidhi biashara zote kwa
kampuni ya udhamini, ambayo itaziendesha biashara hizo huku mtumishi
mwenye mali, akipewa taarifa chache kuhusu biashara yake kwa mwaka.
Pili
mali na biashara ambazo kiongozi wa umma atakuwa nazo, ambazo zinaweza
kusababisha mgongano wa maslahi, atatakiwa kuziuza kabla ya kukubali
kazi ya kutumikia umma au kampuni ya udhamini, inaweza kuuza mali hizo
bila hata kumpa taarifa.
Miongoni
mwa viongozi wa kwanza kuzungumzia mapendekezo hayo, ni marais
wastaafu; Mzee Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili na Benjamin Mkapa, wa
Awamu ya Tatu.
Akizungumza
sheria hiyo, Mzee Mwinyi, alisema Azimio la Arusha, lililokuwa na
miiko ya uongozi, iliyosimamia maadili ya viongozi wa umma halikufutwa
kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali lilizimuliwa ili kuwapatia
viongozi uwezo wa kumudu makali ya maisha.
Alisema
lakini tofauti na matarajio, viongozi walitumia vibaya nia njema ya
Serikali kwa kuanza kumiliki mali hata kwa njia zisizo halali na
kuongeza; “tuliwaruhusu kuingiza mkono, lakini wao wakaingiza mwili
mzima.”
Naye
Mkapa juzi alipokuwa akizungumzia mapendekezo hayo, alisema mtumishi au
kiongozi wa umma anayedhani kuwa sheria hiyo ni kandamizi, huenda akawa
na tatizo la kutumia vibaya mamlaka ya umma.