WAMBURA AFOJI BARUA KUJINUSURU SIMBA

Na Sweetbert Lukonge na Hans Mloli
MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Damas Ndumbaro, amesema wazi kuwa aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais klabuni hapo, Michael Wambura, alifoji barua iliyoonyesha kuwa amerudishiwa uanachama wake.

Hatua hiyo inakuja baada ya Wambura kuwasilisha barua tatu zilizoonyesha aliwahi kusimamishwa na uongozi wa Simba, kisha ukamsamehe zikiwa kama ushahidi wa kujitetea na mapingamizi aliyowekewa katika uchaguzi wa Simba unaotarajia kufanyika Juni 29, mwaka huu ambapo sasa imegundulika kuwa kiongozi huyo alidanganya.

Imeelezwa kuwa Wambura alisimamishwa uanachama wake Simba baada ya kuipeleka klabu hiyo mahakamani mwaka 2010.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili kwenye Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jijini Dar, Ndumbaro alisema barua aliyoiwasilisha Wambura kuwa alisamehewa, imefojiwa kwa kuwa Katibu Mkuu wa Simba wakati huo, Evodius Mtawala amekana kutia saini ya barua hiyo.

“Moja ya barua zile tatu zilizoonekana zina utata, ile ya mwisho ya Septemba 25, 2012 iliyoonyesha kuwa Wambura amesamehewa inaonekana dhahiri imefojiwa kwa sababu tumemuuliza Mtawala na amesema hii si saini yake iliyopo kwenye hii barua.

“Kwa hiyo utaona moja kwa moja kuwa barua hii Wambura aliifoji na wala haikuwa halali kutoka Simba na hili ni kosa kisheria,” alisema Ndumbaro ambaye ni Mwanasheria kitaaluma.

Mei 25, mwaka huu ambayo ilikuwa ni siku ya wagombea kujibu mapingamizi yao, Wambura aliwasilisha barua tatu zinazomwonyesha kuwa yeye ni mwanachama halali baada ya kusamehewa kutokana na kuipeleka Simba mahakamani lakini baadaye zilileta mkanganyiko kutokana na kupishana kwa tarehe za maombi na majibu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo