ZOEZI la kuondoa wafanyabiashara ndogo katika sehemu mbalimbali jijini
Dar es Salaam, imedaiwa haliwezi kufanikiwa kirahisi kutokana na baadhi
ya wafanyabiashara hao kugoma kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa, na
kuwa suluhisho pekee ni wao kutafutiwa maeneo mazuri ya kufanyia
shughuli hizo.
Wafanyabiashara hao ambao awali waliondolewa kufanya biashara zao
katika maeneo yasiyoruhusiwa na Askari waliokuwa wakisafisha jiji,
wameonekana kurudi katika maeneo hayo na kuendelea na shughuli zao kama
kawaida katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Wakizungumza, baadhi yao wamedai kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
wafanyabiashara ni machache hivyo yanachukua wafanyabiashara wachache,
jambo ambalo linakuwa vigumu kwao kwani ndiyo sehemu pekee ambayo
wanatafutia riziki.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Joseph Alphones, anayefanya shughuli zake
katika eneo la Buguruni, alisema kitendo cha wao kuondolewa katika
maeneo yaliyokatazwa bila kuonyeshwa maeneo yanayoruhusiwa si sahihi na
hivyo kusema wanalazimika kurudi katika maeneo ili kuishinikiza serikali
kubadili mawazo iliyotoa hapo awali.
Naye Sophia Samsoni wa Mwenge,
alisema licha ya wao kutegemea maeneo hayo kwa kujipatia riziki,
serikali inatakiwa ione umuhimu wa kuongeza maeneo zaidi ambayo wanaweza
kufanya biashara zao ili kuepusha wizi na uporaji ulioanza katika
maeneo mbalimbali ya jiji hilo kutokana na tamko lililotolewa na baadhi
ya vijana kukosa kazi na kuamua kujiingiza katika wizi.
Mfanyabiashara mwingine
aliyejitambulisha kwa jina la Mama Asumani, wa Ilala alisema, katika
suala hilo linatakiwa kuangaliwa na idara mbalimbali serikalini ili
waweze kusaidika badala ya kuwatimua katika maeneo hayo.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa
Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, amesema hawezi kuzungumzia suala hilo
kwamaana yuko safarini kwa sasa hadi atakaporudi, ambapo katika hatua
nyingine alisema manispaa hiyo katika kipindi cha mwaka jana ilibaini
kuwa wafanyabiashara 21,500 hawana maeneo ya kufanyia biashara.
Afisa habari wa Manispaa ya Temeke,
Joyce Msumba, alisema manispaa hiyo inatarajia kujenga soko jipya la
kisasa lenye hadhi ya wilaya ambalo litatumiwa na wafanyabiashara ndogo
na hivyo kutatua kero inayolalamikiwa mara kwa mara.
Kumbukumbu zinaonyesha
kuwa, utekelezaji wa mpango huo unazingatia sheria ya mipango miji Na. 8
ya mwaka 2007 na sheria ya mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 ambapo maeneo
yaliyotajwa kutoonekana biashara yeyote ni pamoja na Keko, Sandali,
hang’ombe, Kurasini, Mibulani na kata ya Gerezani zote za manispaa ya
Temeke.
Maeneo mengine ni pamoja na Kisutu, Kivukoni, Upanga Mashariki,
Mchafukoge, Kariakoo, Mchikichini, Jangwani, na Upanga Magharibi ambayo
yako katika manispaa ya Ilala na kata za Hananasif, Kinondoni, Kigogo,
Mzimuni na Magomeni zote za manispaa ya Kinondoni.

