Asilimia tisini ya Twiga wote waliopo katika mbuga ya wanyama ya
Ruaha wameathiriwa na ugonjwa unaosambaa kwa kasi ambao haujulikani,
kimeripoti Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
Taarifa zinasema kuwa wanasayansi wa chuo hiko wakishirikiana na
Mamlaka ya Mbuga ya Wanyama Tanzania (TANAPA) wanapambana kuzuia ugonjwa
huo ambao tayari umeshaonekana kwenye mbuga nyingine ya Tarangire.
Profesa Gerald Msinzo, alisema ugonjwa husababishwa na bakteria na
uligunduliwa na maafisa wa TANAPA, ambapo wameonya kuwa hatua za haraka
zinapaswa kuchukuliwa kwani wanyama hao ambao ni kielelezo cha taifa na
kwa sasa wapo katika hatari kubwa.
Alisema kuwa ugonjwa huo una dalili za kuwadhoofisha wanyama, kutokwa
kwa vipele kwenye ngozi zao ambavyo hugeuka kuwa vidonda na majeraha
kwenye miguu yao.
“Ugonjwa huwadhoofisha Twiga na kudhuru uwezo wao kutoka sehemu moja
kwenda nyingine na hivyo kuathiri ulaji wao na hata tabia za
kushirikiana na wanyama wengine” alisema Profesa Msinzo.
Pia aliongeza kwamba vinasaba wa bakteria wanaosababisha ugonjwa huo
vimeshapelekwa kwenye maabara za chuo kikuu kwa ajili ya uchunguzi ili
kutambua ugonjwa na kupata tiba yake.
Hata hivyo, hakuna taarifa kuwa ugonjwa huo unaweza kusambaa na
kuweza kuambukiza viumbe wengine kama wanyama, mimea na hata binadamu