MWENYEKITI wa serikali ya kijiji cha Isenegeja kata ya Mwisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ahmad Jambeck anatuhumiwa na wananchi kutafuna zaidi ya Sh milioni 30 zilizolipwa na kampuni za simu za Airtel, Vodacom na TTCL.
Wakizungumza kijijini hapo, baadhi ya wananchi na wajumbe wa serikali ya kijiji hicho walisema mwenyekiti huyo alianza kula fedha hizo tangu mwaka 2008.
Paulo Elias ambaye ni miongoni mwa wajumbe, alisema pamoja na kampuni hizo za simu kujenga minara ya mawasiliano katika kijiji chao na kulipa fedha kila mwaka, lakini fedha hizo amekuwa akizichukua mwenyekiti wao bila wao kushirikishwa, hata wanapohoji kwenye vikao hufokewa na mwenyekiti huyo.
Rajabu Mohamed alisema mwenyekiti wao amekuwa akiwagawa hata wajumbe wa serikali ya kijiji kwa kuwapa vitisho pindi wanapojaribu kuulizi mikataba ya kampuni hizo. Juma Kimbulu ameutupia lawama uongozi wa wilaya kwa kushindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwenyekiti huyo pamoja na wao kupeleka malalamiko hayo.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Mwisi, Mhogo Rajabu alisema hivi sasa wananchi wa kijiji hicho cha Isenegeja wamekosa imani na mwenyekiti wao kwa sababu ya kuliwa kwa fedha zao na kusababisha kijiji hicho kutokuwa na maendeleo kwa zaidi ya miaka minane na kuiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya mwenyekiti huyo.
Kutokana na tuhuma hiyo, gazeti lilimtafuta mwenyekiti huyo, Ahmed Jambeck ambapo alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwenye kampuni hizo huku akishindwa kutoa idadi ya fedha alizopokea kwa kipindi cha zaidi ya miaka minane.
Aidha mwenyekiti huyo alibainisha kuwa fedha alizopokea zilitumika kujenga vyumba vya madarasa vinne, ofisi moja, stoo moja, matundu 24 ya vyoo, misingi miwili ya majengo katika shule ya msingi Isenegeja pamoja na ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya sekondari Mwisi.
Sambamba na hayo Jambeck alisema tangu achaguliwe mwaka 1999 hakuna mwananchi yoyote aliyewahi kuchangishwa fedha za mchango ya shughuli za maendeleo katika kijiji hicho na ndio maana kila uchaguzi unapofika wamekuwa wakimchagua kwa kura nyingi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Igunga, Revocatus Kuuli amekiri kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambapo alisema alituma mkaguzi wa hesabu na kugundua upotevu wa Sh milioni 34, huku Sh milioni 42 zikionesha zimetumika pasipokuwa na viambatanisho vya matumizi yake na kusema kuwa tayari suala hilo amewakabidhi takukuru kwa hatua zingine.
Mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo alisema tuhuma hizo amezipata kutoka kwa wananchi, tayari amevikabidhi vyombo husika vishughulikie.
Chanzo:Habari leo