WATU 22 walithibitishwa kuaga dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne
katika Kaunti za Embu na Kiambu nchini Kenya baada ya kubugia pombe iliyokuwa na
kemikali hatari ya Methanol.
Waathiriwa 17 waliaga dunia
katika Kaunti ya Embu huku wengine wanne wakiripotiwa kuaga dunia katika
Kaunti ya Embu, visa ambavyo vilitokea chini ya masaa 12.
Walevi hao walikuwa wamebugia
kileo hicho katika kijiji cha Shauri Yako cha Kaunti ya Embu huku wenzao
katika Kaunti ya Kiambu wakikumbana na mauti katika mtaa wa Gwagate.
Katika kisa hicho, watu wengine
52 walilazwa hospitalini wakiwa hawajielewi baadhi yao wakiandamwa na
tishio la kupoteza uwezo wa kuona.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya
kupambana na ulevi na mihadarati (Nacada) Bw John Mututho alilaani visa
hivyo akisema waliozembea kazini wataandamwa pia.Alisema kemikali ya
Methanol hutumika kuandaa pombe za kimaabara lakini lazima ichanganywe
na vipimo vingi vya maji.
"Inaonekana kuwa kemikali hiyo
ambayo kwa matumizi ya binadamu bila kuzingatia vipimo vya maji ni sumu
iliuzwa moja kwa moja kwa waathiriwa," akasema.
Maafisa wa usalama katika Kaunti
hizo walisema kuwa wanafuatilia kiini cha pombe hiyo huku sampuli zake
zikiwasilishwa kwa maabara ya serikali kuchunguzwa.
Mwanamke mmoja aliyetambuliwa
kama Nancy Wairimu alitiwa mbaroni katika Kaunti ya Kiambu akisemekana
kuwa ndiye alikuwa akisambaza pombe hiyo.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kiambu
Bi Esther Maina, mwanamke huyo anazidi kuhojiwa ili kubaini alichotoa
kileo hicho na mbona akakisambaza akijua alikuwa akifanya hivyo kinyume
cha sheria.
"Tunataka kujua ni kwa nini pombe hiyo ikauzwa katika kichaka na alikuwa amekitoa wapi," akasema.
Maumivu makali
Katika Kaunti ya Embu waathiriwa
35 walikimbizwa katuika hospitali kuu ya Embu wakiwa na maumivu makali
huku wengine wakilalamika kuwa walikuwa na shida ya kuona.
Kwa mujibu wa afisa msimamizi wa
hospitali ya Embu Bw Gerald Ndiritu, waathiriwa hao wote walikuwa
wamekunywa kileo hicho mwendo wa saa mbili za usiku kwa kuwa
waliwasilishwa hospitalini mwendo wa saa tatu usiku.
"Wote walikuwa wanalia kwa
maumivu huku baadhi yao wakisema walikuwa wakihisi kiu ya ajabu.
Tunaendelea kuwachunguza na kuokoa maisha yao," akasema.
Bi Maina alisema kuwa walioaga
dunia katika Kaunti ya Kiambu walizirai katika kichaka walikokuwa
wakinywa pombe hiyo na kisha kuaga dunia.
"Wanne kati yao waliaga dunia
ndani ya kichaka hicho huku mwingine akiaga dunia akiwa ndani ya
ambulensi. Wa mwisho aliaga dunia akiwa katika hospitali ya Nazareth
alipokuwa akitibiwa," akasema.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo Bw Elphas Korir alisema kuwa tayari uchunguzi umeanza ukilenga waliokuwa wakisambaza pombe hiyo.
"Kwa sasa tuko na mshukiwa mmoja
mbaroni na tunashirikiana na wenzetu wa Kiambu kujua kama pombe iliyoua
huko ndiyo pia imetutembelea na mauti," akasema.
Bi Maina alisema kuwa machifu na
manaibu wao katika eneo lililoathirika wameamrishwa kuandaa taarifa ya
yale wanayojua kuhusu kisa hicho.
"Tayari tumewachisha machifu saba
kazi kufuatia visa vya pombe haramu kukithiri katika mitaa yao. Hata
katika suala hili, atakayeangukiwa na laweana hatakuwa na budi ila tu
kufutwa," akasema.
