MWANAUME WA MIAKA 34 ALIYETAKA KUJIUA KWA KUJICHOMA VISU 3 KISA MAPENZI, KUFIKISHWA MAHAKAMANI BAADA YA KUPONA

MWANAMUME wa miaka 34 katika Kaunti ya Murang’a Kenya anapokea matibabu chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi ambao wanangojea apone ili wamshtaki kwa kutaka kujitoa uhai kutokana na  mapenzi yake kwa mama wa miaka 48.
Mwanamume huyo alidaiwa kuwa alijichoma visu vitatu tumboni kwa nia ya kujiua baada ya kushuku kuwa kipenzi chake kilikuwa kikigawa mapenzi nje ya uhusiano wao.

Ilibidi maafisa wa polisi waftyatue vitoa machozi ndani ya nyumba yake ili wamzime kujiua huku majirani wakisaidia kuvunja mlango ili kumnusuru.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Kangema Bw Juma Mashua, kisa hicho kilitokea usiku wa kuamkia jana katika eneo la Githiga.

“Mwanamume huyo alirejea kutoka Jiji la Nairobi mwendo wa saa tatu usiku na akapata bibi huyo ambaye ni mhudumu wa baa akiwa hajafika nyumbani. Alisubiri kwa masaa kadhaa na akafahamu kuwa bibi hangerejea,” akasema.

Ilidaiwa kuwa mwanamume huyo alifululiza hadi katika baa ambayo bibi huyo alikuwa  akihudumu na akapata kuwa hakuwepo pia.

“Alirejea nyumbani na akaomba hifadhi kwa jirani yake ambako alilala hadi asubuhi,” akasema Bw Mashua.

Mwendo wa saa kumi na moja asubuhi,  bibi alijitokeza na ndipo jamaa akamfuata hadi ndani ya nyumba.

“Ubishi ulizuka kati yao wawili na ndipo kwa hasira mwanamume huyo alifunga mlango kutoka ndani na kisha akatwaa kisu cha kuchonga viazi na akaanza kujidunga kwa tumbo akilia kuwa hangevumilia kushiriki mapenzi ya uongo,” akasema afisa huyo.

Kuvunja mlango
Nduru za mwanamke huyo ziliwaleta pamoja majirani ambao walipiga simu kwa maafisa wa polisi na kwa bahati njema, kukawa nao walikuwa karibu na eneo hilo.

“Maafisa waliwasili na walipochungulia kwa dirisha, wakapata mwanamume huyo aking’ang’ana na bibi yake aliyekuwa akijaribu kumpokonya kisu hicho,” akasema.

Ni katika hali hiyo ambapo maafisa hao walirusha vitoa machozi ndani ya nyumba hiyo ili kusambaratisha njama ya mwanamume huyo ya kuzidisha majeraha yake huku majirani wakivunja mlango na kumtoa nje.

“Tulimkimbiza hadi hospitali ya Kangema ambapo madaktari wanaendelea kuokoa maisha yake huku nasi tukishika doria  kando ya kitanda chake ili tu akipata nafuu tumchukue na kumfikisha mahakamani kwa nia ya kutisha maisha ya bibi yake na pia kujaribu kujiua,” akasema.

Aliongeza kuwa hiyo ilikuwa mara yake ya pili ya kutekeleza uhalifu huo akitumia kisu kwa kuwa ashawahi kufungwa jela kwa kudunga mpenzi wake mwingine wa awali kwa madai ya kutoaminika katika ndoa.

Via swahilihub


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo