WANAUME WATATU WAUAWA KINYAMA MKOANI MWANZA

Mauaji ya kinyama yametikisha Mkoa wa Mwanza baada ya miili ya wanaume watatu ambao majina yao hayajafahamika wala makazi yao, kukutwa  imefichwa kwenye  vichaka vilivyopo kitongoji cha Kijinga Kijiji cha Igaka wilayani hapa Mkoa wa  Mwanza.
Miili hiyo ilikutwa jana asubuhi kwenye vichaka hivyo baada ya kuuawa kwa kipigo na kunyongwa shingo na watu wasiofahamika usiku wa kuamkia jana.

Inadhaniwa kuwa huenda  walikuwa ni wafanyabiashara wa ng'ombe au wezi  kutokana na   mauaji  yao kufanyika usiku  wa kuamkia siku ya mnada wa ng'ombe kwenye kijiji jirani cha Sima kilichopo wilayani hapa.

''Miili yao imeharibiwa kwa kipigo na ina majeraha kiasi cha kuharibika lakini bado inaweza kutambuliwa....  inawezekana wapo wanaoweza kuwafahamu lakini wanasita maana bado haijafahamika  wameuawa katika mazingira gani, '' amedai mmoja wa watu walioshuhudia miili hiyo wakati akizungumza na NIPASHE mnadani hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlolowa alithibitisha miili  hiyo kukutwa katika  vichaka vilivyopo kwenye kitongoji hicho kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Sengerema na Geita.

Mlolowa alisema miili hiyo imehifadhiwa katika hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema baada ya juhudi za kuitembeza baadhi ya maeneo yenye mikusanyiko ya watu yakiwamo ya kwenye mnada huo wa Sima, Soko Kuu na kituo cha mabasi Sengerema kutotambuliwa.

 Alisema inaonyesha kuwa huenda watu hao waliuawa katika eneo jingine na kutupwa kwenye vichaka hivyo.

Kamanda huyo alisisitiza kuwa bado wanaendelea kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu hao waliouawa, sababu za mauaji na wauaji wao.

CHANZO:NIPASHE


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo