MKAZI wa Kijiji cha Ibindi, Tarafa ya Nsimbo, wilayani Mlele, Michael
Silanda (26), amefariki dunia baada ya kunywa pombe za viroba aina ya
Zed kupita kiasi bila kula.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema tukio
hilo lilitokea Mei 5 mwaka huu, saa 6 usiku kijijini hapo.
Alisema siku ya tukio, Silanda alikwenda baa na kuanza kunywa pombe
hiyo bila kula kitu chochote hadi saa 6 usiku alipoamua kurudi nyumbani
kwake huku akiwa amelewa kupita kiasi.
“Baada ya kufika nyumbani kwake aliingia ndani na kulala bila kula na
siku iliyofuata saa 2 asubuhi ndipo walipomkuta akiwa amefariki
dunia,” alisema.
Kamanda Kidavashari alisema uchunguzi wa awali umebaini kifo hicho
kimesababishwa na Silanda kunywa pombe kupita kiasi bila kula
chakula.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa
kufanyiwa uchunguzi na utakapokamilika watakabidhiwa ndugu kwa mazishi.
Na Walter Mnguluchuma
