Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo ameeleza wazi Msimamo wa Chama hicho katika Sekta ya Elimu, kwa kubainisha kuwa maono ya CCM ni kuona Tanzania kama Taifa linakuwa na mitaala ambayo itatoa Elimu ya Taaluma ya Kujiajiri kuliko Kutegemea Ajira kwa Sekta ya Umma ama Binafsi.
Chongolo amebainisha Msimamo huo Leo Mei 28, 2023 alipokuwa akizungumza na Wananchi pamoja na Wana CCM katika Kata ya Malangali ambayo ipo katika Jimbo la Mufindi kusini mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 7 mkoani humo ikilenga kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020/2025 pamoja na Kuzungumza na Makundi mbalimbali ya Kijamii.
Amesema tayari Mwenyekiti wa Chama hicho ambae ni Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatoa idhini kwa kamati ambayo imekabidhiwa Jukumu la kupitia na kuangalia Upya mfumo wa Elimu ili kuja na mapendekezo ya Mitaala itakayokidhi soko la Ajira katika Muktadha wa Kujiajiri baada ya kumaliza masomo kuliko kutegemea Ajira Pekee.
Aidha Katibu mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo, amesema Serikali imeweza kutatua Changamoto ya pembejeo kwa Wakulima, ikiwemo suala la mbolea ambapo kwa imeweka ruzuku na hivyo kufanya bei kushuka na hivyo wakulima wengi kumudu kununua.
"Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kushughulikia upatikanaji wa Pembejeo kwa njia ya haraka Urahisi, ambapo kazi kubwa iliyobaki kwa Wakulima ni kuendelea na kilimo chenye tija kwa kuwa Changamoto zingine kwenye Sekta ya Kilimo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi wa Kudumu" amesema Chongolo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Ndugu Daud Yasin (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini (CCM) Ndugu David Mwakiposa Kihenzile pamoja na Viongozi na wanachama wengine wakitembea kwa miguu kuelekea Nyololo kuhudhuria kikao cha shina namba 27, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku 7 mkoani Iringa .
Katibu Mkuu ameongozana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi Gavu na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema.