MKUU wa Wilaya (DC) ya Kiteto mkoani Manyara, Martha Umbulla, amedaiwa kuwa chanzo cha kuchochea mauaji ya wakulima na wafugaji.
Madai hayo yalitolewa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na
mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) wakidai anaendesha
utawala wa kibaguzi.
Akizungumza kwa hasira muda mfupi kabla ya kusitisha Bunge kwa ajili
ya mapumziko ya mchana jana, Ndugai alisema mauaji hayo sio ya wakulima
na wafungaji, bali ni ya kikabila kama yale ya Rwanda na Burundi.
Kauli ya Ndugai ilifanana na ile ya Lema ambaye alikuwa wa kwanza
kuwasha moto kwa kusema mauaji hayo yanatokana na utawala wa kibaguzi
unaofanywa na Umbulla ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu.
Kwa mujibu wa Lema, utawala wa kibaguzi wa DC huyo, hauna tofauti na
ule wa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck ole Medeye (CCM).
Alisema kuwa kinachotokea Kiteto na kusababisha wakulima na wafugaji
kuuana, ni viongozi kujenga misingi ya ubaguzi ambao unafanywa na
watawala wa maeneo husika.
“Ukiona watawala wanaanza kufanya mikutano kwa ajili ya kuwabagua
watu, ujue moja kwa moja kuwa hali haiwezi kuwa nzuri na ndiyo maana
mauaji yanajitokeza.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kukupa pole wewe
mwenyewe kuwa mpaka jana usiku, nimepigiwa simu kuwa watu wawili ambao
ni wakulima wa Kiteto wamekufa, pikipiki 11 na trekta moja vimechomwa
moto na wamechoma maduka.
“Kwa sababu hivi karibuni DC alifanya mkutano wa wananchi, akasema
kuwa wale wageni wakae kushoto na wenyeji wakae kulia. Ni hatari zaidi
katika nchi, ni sawa na kusema kama ni vita na viendelee. Hivyo, suala
hilo liangalie kwa makini,” alisema Lema.
Hata hivyo, tuhuma za Lema ziliibua hasira za Medeye na kuomba
mwongozo wa spika kwa kuomba kama kuna uwezekano kuwepo kwa daftari la
kuwaorodhesha wote ambao wanaonekana kuwa na matatizo ya akili ili
wajulikane.
“Godbless Lema, mtoto aliyekulia kwenye gheto kwa sababu ya
kutelekezwa na wazazi wake, alipata huruma pale Arusha akapata ubunge,
kama wana Arusha wangekuwa na ubaguzi ungepataje ubunge wewe?” alisema
Medeye na kutishia kwamba uchaguzi mkuu ujao atagombea ubunge jimbo la
Lema kwa sababu ndiko alikozaliwa.
Kauli ya Lema iliungwa mkono na Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM),
ambaye alisema kuwa kimsingi hawezi kuunga mkono hotuba ya waziri
yeyote kwani wengi hawatimizi wajibu wao.
Alisema kuwa imekuwa mazoea kwa mawaziri kufika katika Jimbo la Gairo
na kuwaahidi wananchi kuwa watapeleka maji, lakini hakuna
kinachofanyika.
Mbali na hilo, alisema kuwa kitendo cha wakulima kuuawa katika eneo
la Kiteto, ni kutokana na ubaguzi ambao unafanywa na viongozi kutokana
na kuwabagua wakulima na wafugaji, huku wakisingizia kuwa eneo
wanalolima ni hifadhi.
Akitoa utetezi wake, Umbulla alisema mkutano alioufanya katika Kijiji
cha Kimana wilayani Kiteto ulikuwa ukiwalenga wanakijiji hicho tu.
“Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mbunge aliyemaliza kuzungumza,
mheshimiwa Lema, kuwa mkutano nilioufanya ulikuwa unalenga wananchi wa
Kijiji cha Kimana tu kutokana na wakulima kutoka Kongwa na Chemba kuwa
na tabia ya kutuvuruga, na Lema asipende kuingia katika mambo ambayo
naye anapenda kutuvuruga,” alieleza Umbulla.
>>>Tanzania daima
