WAKATI wadau wa elimu wakitupia lawama kwa wanafunzi na wazazi,
wanafunzi mkoani Manyara wamewalaumu walimu wao kwa kutokuwa na
mahusiano mazuri wawapo shuleni.
Wakizungumza kwenye mkutano wa maadhimisho ya Juma la Elimu za Msingi
na Sekondari, baadhi ya wanafunzi walisema walimu wao hasa wa masomo
ya Hisabati na Sayansi wamekuwa na tabia ya ukali wanapokuwa darasani,
hivyo kuwafanya wafikie hatua ya kuyachukia masomo hayo.
Walisema walimu wao wanashindwa kuwapa msaada pindi wanapotaka kuhoji
jambo ambalo halijaeleweka katika somo husika badala yake wanatoa
lugha za ukali na kuwakatisha tamaa ya kusoma.
“Mahusiano yetu na walimu wetu hasa wa somo la Hisabati na Sayansi ni
mabaya kutokana na wao kuwa wakali na kutufanya tushindwe hata kuuliza
maswali, tunaomba wabadilishe mfumo wa ufundishaji, wasiwe wakali ili
tuwe karibu nao, pia tuwe huru kueleza shida zetu kwao,” alisema
mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari.
Hata hivyo, walibainisha kwamba kuna tabia ya baadhi ya wazazi/walezi
wenye watoto wao wanaosoma katika baadhi ya shule wilayani humo
kuwakatisha tamaa walimu ambao wamekuwa kipaumbele kufuatilia mienendo
ya wanafunzi hao.
Kwa upande wa wadau hao, walieleza wanafunzi wengi wanafeli kutokana
na kutokuwa makini na kuzingatia kile walichokifuata shuleni, badala
yake wamekuwa wakiendekeza anasa.