Wakuu wa tume ya uchaguzi nchini Afrika-Kusini
wametangaza kuwa shughuli ya kuhesabu kura inaenelekea kukamilika baada
ya uchaguzi mkuu uliofanyika juzi kwa mara ya tano tangu utawala wa
mwafrika mzungu.
Chama tawala cha ANC kinaongoza kwa zaidi ya asilimia 63, huku kile cha Democratic Alliance kikiwa na asilimia 23.
Chama kipya cha Economic Freedom Fighters cha Julius Malema kikiwa katika nafasi ya tatu.
Jumla ya asilimia 96 ya kura zilizopigwa zimehesabiwa.
Mwandishi wa BBC Andrew Harding anasema kuwa
ukosefu wa ajira,ufisadi na ukosefu wa usawa katika jamii ni changamoto
kubwa lakini wapiga kura bado wana imani na chama cha ANC.
Tume ya uchaguzi imesema kuwa uchaguzi
ulifanyika kwa amani katika maeneo mengi ya nchi huku asilimia 73 ya
wapiga kura wakijitokeza kupiga kura.
Uchaguzi huu ni wa kwanza tangu nchi hiyo
kuondokewa na rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo hayati Nelson
Mandela. Afrika Kusini imetimiza miaka 20 tangu kumalizika kwa utawala
wa wazungu.
Idadi kubwa ya wananchi imekuwa ikilalamikia utenda kazi wa serikali hasa kwa kuwa kuna kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira.
Wadadisi wanasema kuwa chama cha ANC huenda
kikatumia fursa hii kuimarisha uchumi wa nchi hasa baada ya miaka mitano
ya kile kinachosemekana kuwa utawala mbovu wa Rais Jacob Zuma.
BBC
